HRW: Msumbiji ichunguze dhuluma za kingono
25 Februari 2016Watu wasiopungua 6,000 tayari wameyakimbia makaazi yao kwenye mkoa huo na kukimbilia taifa jirani la Malawi tangu Oktoba 2015 wakati majeshi ya serikali yalipoanza operesheni ya kuwapokonya silaha wapiganaji wanaohusishwa na chama cha upinzani cha RENAMO.
Wakimbizi kadhaa waliozungumza na Human Rights Watch (HRW) katikati ya Februari 2016, wanasema walitoroka makwao kutokana na unyanyasaji unaofanywa na majeshi na wanaogopa kurudi. Mkoa wa Tete ambao una utajiri wa makaa ya mawe na unaopakana na Malaawi ni ngome kuu ya RENAMO.
Wanawake kadhaa walielezea jinsi walivyowaona wanajeshi wakiwaua waume zao na wanakijiji wengine, huku wakiwafunga wengine pingu au kamba na kuwapeleka kusikojulikana. Katika visa vingi, wanajeshi walichoma moto nyumba, maghala na mashamba wakiwalaumu wakaazi wa maeneo hayo kwa kuwalisha na kuwaunga mkono wapiganaji wa RENAMO.
Zenaida Machado, mtafiti wa HRW, anasema wanajeshi hawapaswi kutumia kisingizio cha kupokonya wapiganaji silaha kama sababu ya kufanya maovu dhidi yao au dhidi ya wakaazi, akiongeza kwamba "serikali inapaswa kuanzisha uchunguzi ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanyika kwa kufuata sheria."
Hali ya taharuki imeendelea kutanda kati ya chama kinachotawala, Mozambique Liberation Front - FRELIMO, na kile cha upinzani, Mozambique National Resistance - RENAMO, tangu Oktoba 2014 baada ya FRELIMO kushinda uchaguzi mkuu nchini humo.
Awali RENAMO ilishaanza mapigano japo kwa kiwango kidogo miongo miwili baada vita vibaya vya wenyewe kwa wenyewe. Mnamo mwaka 2014, mkataba wa amani ulitiwa sani, lakini RENAMO inasema serikali imekataa kujumuisha wapiganaji wake kwenye vikosi vya jeshi kama walivyoafikiana. Kwa upande wake, serikali inasema chama cha RENAMO kimekataa kuwasilisha majina ya wapiganaji wake wanaopaswa kujumuishwa kwenye jeshi la serikali.
'Mume wangu aliuawa mbele ya macho yangu'
Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 20 kutoka kijiji cha Ndande anasema mnamo tarehe 7 Februari 2016, wanajeshi watano wa serikali waliivamia familia yake na kuilaumu kwa kulilisha kundi la wapiganaji wa RENAMO.
"Wanajeshi walimtesa mume wangu na kisha kumpiga risasi mbele yangu," anasema mwanamke huyo, ambaye baadaye alitoroka siku hiyo hiyo akiwa na wanawe wawili na kujificha kwenye kingo za Mto Mpandwe, na usiku ulipowadia akavuuka mpaka kuingia Malawi.
Mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 33 anasema alichapwa mijeledi na kuzuiliwa kwa masaa kadhaa na wanajeshi tarehe 5 Februari katika eneo la Ncondezi wilaya ya Moatize.
"Wanajeshi walisema mimi ni mwizi na mwanachama wa kundi la wapiganaji la RENAMO", anaelezea. Naye pia alifanikiwa kutoroka na kukimbilia Malawi.
Shahidi mwengine anasimulia jinsi siku moja katka mwezi Disemba 2015, wanajeshi walipomshika mtu waliyedai kuwa mpiganaji wa RENAMO katika kijiji cha Madzibawe, kisha wakamfunga kamba shingoni na kuikata sehemu ya shingo kwa panga na kumjeruhi vibaya.
Madai ya wanajeshi kukiuka haki za binadamu pia yametolewa na mzee mmoja kwa jina Ndande mwenye umri wa miaka 74, na ambaye sasa ni mkimbizi kwa mara ya pili nchini Malawi. Anasema mwezi Januari 2016, wanajeshi waliichoma moto nyumba yake "na kila kitu hadi mashamba."
Shirika la Human Rights Watch pia lilipokea ripoti za dhuluma za kimapenzi zinazofanywa na vikosi vya jeshi la Msumbiji. Hata hivyo, wengi wa waathiriwa walichelea kuripoti kwa kuhofia unyanyapaa.
Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 19 na ambaye sasa ni mjamzito anasema wanajeshi walimwamuru alale chini na kugusa nyeti zake "Kwa kutumia fimbo kwa njia isiyofaa."
Malawi yataka wakimbizi warudi Msumbiji
Tarehe 18 Februari, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) liliripoti kuwa zaidi ya watu 6,000 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto - walisajiliwa kama waomba hifadhi katikati ya mwezi Disemba 2015 katika kambi za Kapise na Mwanza zilizoko umbali wa mita 300 kutoka mpaka wa Msumbiji. Kambi hizo zina visima viwili tu vya maji na vyoo vinne na hazina shule.
Hata hivyo, badala ya serikali ya Malawi kuwasajili wakimbizi wapya na kuboresha makambi hayo, imewataka warudi makwao. Afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya maswala na usalama wa ndani, Beston Chisamire, aliliambia shirika la Human Rights Watch kwamba Malawi haitashughulika na wakimbizi hao wapya.
Shirika la UNHCR limezihimiza Malawi na Msumbiji kuheshimu haki ya wakimbizi hao wapya.
Maafisa wa serikali ya Msumbiji wameshazuru kambi hiyo mara tatu kuzungumza na waathiriwa wakiwaomba warejee nyumbani, lakini wakimbizi waliozungumza na HRW wanasema hawataki kurejea kwa kuhofia machafuko na kuhangaishwa na vikosi vya serikali. Wanapinga madai ya serikali ya Msumbiji kuwa usalama umerejea na hivyo ni salama kurejea nyumbani.
Mwezi wa Januari 2016, serikali ya Msumbiji ilidai kuwa watu wanaoingia Malawi si wakimbizi bali wakulima ambao huvuka mipaka mara kwa mara. Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Balozi Antonio Matonse, aliliambia shirika la HRW kuwa baada ya wajumbe wa serikali yake kuizuru kambi ya wakimbizi ya Kapise, walifikia uamuzi kwamba "hofu inayotokana na operesheni ya kijeshi, mapigano ya ghafla na ukame zimechangia watu kuhama."
Mwandishi: John Juma/HRW Mozambique
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman