HRW: Uhuru mashakani kuelekea uchaguzi Tanzania
2 Septemba 2020Shirika la Human Rights Watch limesema tangu katikati ya mwezi Juni mwaka huu serikali ya Tanzania imewakamata wanachana wa vyama vya upinzani wapatao 17 pamoja na wakosoaji wa serikali, imesitisha kibali cha shirika moja la kuetea haki za binadamu, imefuta leseni ya shirika lengine moja, na kuyazuia mashirika makubwa ya haki za binadamu yasishiriki mchakato wa kuangalia mwenendo wa uchaguzi kama waangalizi.
Shirika hilo pia linasema maafisa nchini humo wameweka sheria mpya dhidi ya vyombo vya habari, wakifuta leseni ya gazeti moja linalohusishwa na mwanasiasa mmoja wa upinzani na kuvibana baadhi ya vyombo vya habari kwa sababu ya kuripoti kuhusu ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, ambao rais wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli anasema haupo tena katika nchi hiyo.
Oryem Nyeko, Mtafiti mwandamizi wa shirika la Human Rights Watch kanda ya Afrika, amesema sio sadfa kwamba serikali ya Tanzania imeongeza ukandamizaji wa makundi ya upinzani, wanaharakati na vyombo vya habari wakati huu uchaguzi ukikaribia kufanyika. Nyeko amehoji badala ya kuheshimu na kuendeleza haki ya kutoa maoni wakati huu muhimu kwa taifa hilo, maafisa badala yake wamechukua hatua zinazoibua wasiwasi kuhusu ikiwa uchaguzi wa Oktoba 28 utakuwa huru na wa waki.
Katika ripoti yake Human Rights Watch inasema serikali iliwatia mbaroni na kuwazuia kwa muda mfupi wanachama wa vyama vya upinzani, kikiwemo chama cha ACT Wazalendo na chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, kwa misingi ya kuhatarisha amani ya nchi au kufanya mikutano kinyume na sheria. Mwezi Julai mwaka huu polisi walimkamata na kumuzia shehe ya kiislamu, Issa Ponda, kwa siku tisa baada ya kufanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alitoa wito kufanyike uchaguzi huru na wa haki Tanzania.
Ripoti hiyo pia inasema serikali imeweka sheria mpya dhidi ya vyombo vya habari na uhuru wa kutoa maoni kwenye mtandao. Serikali ilipitisha sheria zinazopiga marufuku vituo vya utangazaji Tanzania kushirikiana na vituo vya habari vya kimataifa bila maafisa kutoka kwa Mamlaka ya mawasiliano, TCRA, au wakala mwingine wa serikali kuwepo. Serikali pia iliridhia sheria na kanuni kuhusu uhalifu wa mtandaoni kuhusu masuala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na taarifa zinazochapishwa mtandaoni, ikiwemo kuandaa maandamano au kuutangaza na kuunga mkono ushoga.
Mtafiti mwandamizi wa shirika la Human Rights Watch, Oryem Nyeko, anasema hatua zote zilizochukuliwa katika wiki za hivi karibuni, zinaathiri mazingira ya uchaguzi kufanyika kwa haki. Nyeko aidha amesema ili uchaguzi wa Tanzania uwe huru na wa haki, serikali inahitaji kuyaruhusu mashirika ya haki za binadamu na vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru, na wapinzani wa kisiasa na wakosoaji waachwe watoa maoni yao kwa uhuru.
https://www.hrw.org/news/2020/09/02/tanzania-freedoms-threatened-ahead-elections