1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 30 wamekufa katika maandamano ya kupinga serikali Kenya

29 Juni 2024

Shirika la Human Rights Watch limesema takriban watu 30 walikufa katika maandamano nchini Kenya ya juma hili yaliyochochewa na harakati za serikali kutaka kuongeza kodi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4hf0q
Maandamano ya Kenya mjini Nairobi
Maafisa wa polisi wakimtia mbarini mwandamanaji katika maandamana kupinga mapendekezo ya mswada wa fedha wa Kenya wa 2024/2025, Nairobi, Kenya, Juni 27, 2024.Picha: Monicah Mwangi /REUTERS

Katika taarifa yake shirika hilo limesema "Vikosi vya usalama vya Kenya vilifyatua risasi moja kwa moja kwenye umati wa waandamanaji siku ya Jumanne Juni 25, 2024, wakiwalenga pia baadhi ya waandamanaji waliokuwa wanakimbia."

Pamoja na kwamba hakujawa na uthibitisho wa idadi kamili ya watu waliouawa Nairobi na miji mingine, Human Rights Watch iligundua kuwa watu wasiopungua 30 waliuawa siku hiyo kwa mujibu wa hesabu za walioshuhudia, taarifa zilizopatikana kwa umma, rekodi za hospitali na chumba cha kuhifadhi maiti huko Nairobi.

Lakini kwa upande wake Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya inayofadhiliwa na serikali ilisema kuwa imerekodi vifo 22 na waliojeruhiwa 300, na kuongeza kuwa itaanzisha uchunguzi kufuatia mikasa hiyo.