1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huduma za maji zitabinafsishwa?

Mirjam Gehrke / Maja Dreyer20 Machi 2006

Faida na matatizo ya kubinafsisha huduma za maji – hilo ndilo suala muhimu kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu maji unaoendelea nchini Mexiko. Kando ya mkutano huo, wapinzani wa ubinafsishaji wa huduma za maji wanaendesha kongamano lao chini ya kichwa cha maneno “Kulinda maji”.

https://p.dw.com/p/CHnZ
Hali itakuwa bora baada ya huduma za maji kubinafsishwa?
Hali itakuwa bora baada ya huduma za maji kubinafsishwa?Picha: AP

Moja ya mashirika yaliyoandaa mkutano huo wa kulinda huduma za maji ni shirika la Kijerumani la kutoa msaada “Mkate kwa dunia”. Mwakilishi wake, Annette von Schönfeld, anaeleza sababu za kufanya mkutano huo: “Sisi tunaona mkutano huo mkubwa wa maji unahudhuriwa na kampuni nyingi za kibinafsi. Shirika lililoandika mialiko ni hadhara ya maji duniani. Hadhara hiyo ina mahusiano ya karibu sana na makampuni makubwa ambayo yanafanya biashara ya maji. Sisi lakini tunasema kupata maji ni haki ya kimsingi ya binadamu. Lazima kila mmoja aweze kupata maji bila kuangalia ana uwezo gani wa kuyalipa.”

Ingawa haki ya kimsingi ya binadamu kupata maji inazungumziwa pia kwenye mkutano rasmi wa maji, washirika wa mikutano hii miwili hawatumii lugha moja, anasema Danielle Mitterand, mwenyekiti wa mfuko France Libertés. Shirika lake linadai gharama za kijeshi zipunguzwe ili fedha zaidi zitumike kwa ajili ya kuendeleza miundo mbinu ya maji. Bibi Mitterand anadai kila mtu apewe lita 40 ya maji safi kila siku.

Kwenye mkutano rasmi wa maji jitihada kubwa zinafanywa ili kupatanisha katika majadiliano makali kuhusu kubinafsisha huduma za maji. Wajumbe wengi wanasema siyo maji yenyewe ambayo yanabinafsishwa. Lakini ni huduma za maji, yaani kazi yote ya kupeleka maji kwa utumiaji ambayo huenda ikabinafsishwa ili huduma hizo ziwe bora kuliko zamani.

Annette von Schönfeld wa shirika la “Mkate kwa dunia” lakini haungi mkono haja hiyo: “Ni sawa kwamba mara nyingi kampuni za kibinafsi zinasaidia kwa upande wa kiteknolojia. Lakini ikiwa uchumi wa kibinafsi unashiriki katika biashara hiyo, sehemu kubwa ya uamuzi au mara nyingi maamuzi yote kuhusu namna ya kupanga huduma za maji yanachukuliwa na kampuni hizo. Kwa kawaida, hilo ni sharti linalowekwa na kampuni za kibinafsi. Hivyo, taasisi za kiserikali haziwezi tena kusimamia ugawaji wa maji.”

Ingawa suala la ugawaji wa maji linaziathiri zaidi nchi maskini ambapo huduma za maji bado zinajengwa, kampuni za kibinafsi zinaingia pia katika soko la maji barani Ulaya. Wakati serikali za miji na mikoa zinauza huduma hizo ili kusawazisha bajeti zao, wananchi wanaunda mashirikiano ili kupinga maendeleo haya.