IAEA kuchunguza maeneo ya nyuklia Ukraine
25 Oktoba 2022Grossi amesema jana kwenye taarifa yake kwamba shirika hilo la IAEA limepata maombi kwa njia ya maandishi kutoka kwa Ukraine, ikiomba kupelekwa timu ya waatalamu wa ukaguzi ili kuchunguza shughuli zinazoendelea katika maeneo hayo ambayo hata hivyo hayakutajwa.
Maeneo hayo mawili ya nyuklia yako chini ya uangalizi wa kiusalama wa IAEA na yamekuwa yakitembelewa mara kwa mara na wakaguzi wa shirika hilo, amesema Grossi na kuongeza kuwa walizuru maeneo hayo miezi miwili iliyopita na kila kitu kilikuwa sawasawa na maazimio ya Ukraine yanayohusu usalama wa vinu vya nyuklia na hakukua na vifaa ama shughuli zozote zilizokuwa kinyume na maazimio hayo zilizogundulika kufanyika kwenye maeneo hayo.
Madai ya Urusi kwamba Ukraine inajiandaa kutumia mabomu ya kemikali ya sumu
Amesema, baada ya ombi hilo wakaguzi hao watatembelea maeneo hayo katika siku zijazo kuangalia iwapo kuna uwezekano wa shughuli ambazo hazikutajwa ama vifaa vyovyote.
Taarifa hiyo imetolewa jana jioni wakati kukiwa na madai kutoka Urusi ya kwamba Ukraine inajiandaa kutumia mabomu ya kemikali za sumu, ambayo ina utaalamu wa kuyatengeneza, madai ambayo Ukraine na mataifa ya magharibi yameyapuuzilia mbali.
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewasili jijini Kyiv
Katika hatua nyingine, rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewasili jijini Kyiv mapema leo katika ziara ya ghafla, na ya kwanza kwa kiongozi huyo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine kwa mara ya kwanza Februari 24.
Miongoni mwa mambo anayoyafanya kwenye ziara hiyo ni kukutana na rais Volodymyr Zelenskiy. Kabla ya kukutana naye amewaambia watu wa Ukraine kwenye taarifa yake kwamba, waendelee kuitegemea Ujerumani.
Licha ya msaada wa kijeshi, Steinmeir ameongeza kwamba ziara yake inalenga pia kuangazia namna ya kusaidia ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa kama ya usambazaji wa umeme, mambomba ya kusambaza maji na mifumo ya kusambaza nishati, haraka iwezekanavyo kabla majira ya baridi hayajaanza.
Ikumbukwe uamuzi wa Kyiv wa kuruhusu ziara ya Steinmeier ulitolewa katikati ya ukosoaji wa muda mrefu dhidi yake kuhusiana na mahusiano na Urusi na kushindwa kwake wakati akiwa waziri wa mambo ya kigeni kukabiliana na maonyo yaliyotolewa na majirani wa Ulaya ya Mashariki kuhusiana na kitisho cha uvamizi wa Urusi. Hata hivyo, mvutano huo ulimalizwa mapema mwezi Mei.
Jeshi lawataka raia kuondoka katika eneo la mapigano la Kherson
Na huko kwenye jiji la Kherson linalodhibitiwa na Urusi, jeshi la nchi hiyo limewataka raia wa eneo hilo kuondoka mara moja wakati wakazi wengi wakiungana na wenzao kukimbia uwezekano wa mashambulizi ya kushtukiza ya jeshi la Ukraine. Urusi imesema vikosi vyake tayari vimezuia jaribio la Ukraine la kuvuka mstari wa eneo hili wanalolidhibiti.
Uongozi uliowekwa na Urusi kwenye jiji hilo umetangaza kwamba umeunda kundi la wapiganaji , na kusema wanaume wote wanaosalia wanatakiwa kujiunga nalo.
Kwenye upande wa diplomasia, Urusi inaangazia kupeleka madai yake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hatua ya Ukraine ya kutaka kufanya mashambulizi ya mabomu ya kemikali za sumu, hii ikiwa ni kulingana na wanadiplomasia wa Urusi. Aidha tayari imewasiliana na baadhi ya mataifa ya magharibi kuhusiana na nia yake hiyo.
Soma zaidi:Urusi yaondoa maafisa wake Kherson ikitaraji mashambulizi ya Ukraine
Hata hivyo Uingereza, Ufaransa na Marekani tayari zimesema zitaiunga mkono Ukraine kwa namna yoyote itakavyowezekana, huku yakipinga kabisa maonyo hayo ya Urusi kuhusiana na matumizi ya mabomu hayo ya sumu.
Vyanzo: DPA/RTR