1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

IAEA kufunga Kamera mpya kwenye kituo cha nyuklia cha Iran

16 Desemba 2021

Shirika la kudhibiti nguvu za Atomiki duniani, IAEA limesema limefikia makubaliano na Iran ya kufunga tena kamera katika kituo kimoja cha nyuklia cha nchi hiyo na kumaliza mvutano kuhusu suala hilo.

https://p.dw.com/p/44MEE
Iran Atomkraftwerk Bushehr
Moja ya vituo vya nyuklia vya IranPicha: TASS/picture alliance

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa jana IAEA itafunga kamera mpya na kuondoa zilizoharibika katika kituo cha shughuli za nyuklia cha Karaj ambacho Iran inasema kilihujumiwa mnamo mwezi Juni.

Suala la kufungwa kamera mpya za kufuatilia nyendo kwenye kituo hicho kinachotengeza vifaa vya kuunda mitambo ya kurutubisha madini ya urani limekuwa kitovu cha mvutano wa hivi karibuni kabisa kati ya Tehran, IAEA na madola yenye nguvu yanayotaka kudhibiti mradi wa nyuklia wa Iran.

Tangu shambulizi la mwezi Juni katika kituo hicho cha nyuklia, Iran ilizuia kubadilishwa kwa kamera zilizoharibika uamuzi uliomaanisha kwamba wachunguzi wa IAEA hawakufahamu chochote kilichokuwa kinaendelea.

Grossi: Makubaliano na Iran yanafungua njia ya kuendelea mazungumzo ya Vienna 

Rafael Mariano Grossi IAEA in Iran
Mkuu wa shirika la IAEA Rafael Grossi (kushoto) akizungumza na naibu mkuu wa shirika la nyuklia la Iran Beheouz Kamalvandi mjini TehranPicha: Atomic Energy Organization of Iran/picture-alliance/AP

Mkuu wa shirika la IAEA Rafael Grossi amesema makubaliano yaliyofikiwa jana ni hatua muhimu chini ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 ambao hivi sasa ni kama umeparaganyika.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Grossi amesema watazidi kuyafanyia kazi masuala mengine kadhaa yanayotatiza kusonga mbele kwa mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna ya kujaribu kuufufua mkataba wa nyuklia unaonuwia kuizuia Iran kutumia mradi wake wa nyuklia kuunda silaha nzito.

IAEA imesema kamera mpya zitafungwa katika kituo cha Karaj ndani ya siku chache zinazokuja.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Hossein Amirabdollahian amesema dola hiyo ya Uajemi imefikia makubaliano mazuri na IAEA kuhusu suala la kufuatilia kituo cha Karaj.

Iran imekuwa ikisitasita kuruhusu kufungwa kwa kamera mpya ikidai kwamba huenda data za kamera zilizokuwepo ndiyo zilitumika kupanga na kutekeleza shambulizi la mnamo mwezi Juni dhidi ya kituo cha Karaj ambalo lililoharibu miundombinu muhimu ya eneo hilo.

Madai hayo yalishakanushwa vikali na mkuu wa IAEA Rafael Grossi.

Marekani yaridhika lakini wataalamu watoa tahadhari

Wien, Österreich | IAEA
Picha: Alex Halada/AFP/Getty Images

Makubaliano ya kufungwa tena kamera huko Karaj yanatoa matumaini ya kusonga mbele kwa mazungumzo ya mjini Vienna.

Licha ya makubaliano hayo Iran bado itakuwa na haki ya kutunza taarifa zilizorikodiwa baada ya wataaalamu wa IAEA kwa kushirikiana na maafisa wa Tehran kupembua kile kilichonaswa na vifaa hivyo.

Ijapokuwa makubaliano hayo yamepokewa kwa bashasha na Marekani, wataalamu kutoka mashirika kadhaa wamesema bado yameacha maswali ya msingi yanayoulizwa kila mara kuhusu mkakati wa kufuatilia shughuli za nyuklia za Iran.

Moja ya maswali yanayoulizwa kila mara ni vipi wachunguzi wa IAEA wanaweza kubaini idadi ya mitambo ya kurutubisha madini ya Urani iliyotengenezwa kwa kutumia data za kamera pekee.

IAEA lakini imesema masuala yote hayo yatazingatiwa mara hii.