ICC yaanza vikao vya kila mwaka mjini The Hague
2 Desemba 2024Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya Jinai ICC imefungua mkutano wao wa kila mwaka wakati ambapo mahakama hiyo ikikabiliwa na msukumo juu ya vibali vyake vya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa Ulinzi.
Wawakilishi wa nchi 124 wanachama wa ICC watajumuika mjini The Hague Uholanzi kuanzia leo hadi tarehe 7 katika mkutano wao wa 23 ambao wanatarajiwa kuichagua kamati mpya na kupitisha bajeti ya mahakama hiyo ya ICC.
Mwezi uliopita, waendesha mashtaka walikubali ombi kutoka kwa mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo mwendesha mashtaka Karim Khan kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wake wa zamani wa ulinzi na mkuu wa jeshi la Hamas, akiwatuhumu kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu katika vita katika ukanda wa Gaza.
Soma zaidi. UN: Waandishi wa habari zaidi ya 250 wamekamatwa tangu Taliban ilipoingia madarakani
Hatua hiyo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza kwa kiongozi ambaye ni mshirika mkuu wa nchi za Magharibi ameshtakiwa na mahakama ya kimataifa ya haki. Uamuzi huo ulishutumiwa na wakosoaji wa mahakama hiyo tofauti na hatua kama hiyo iliyochukuliwa na mahakama hiyo dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin mwaka uliopita juu ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.
Ilipotolewa waranti ya kukamatwa kwa Netanyahu na waziri wa ulinzi, Rais wa Marekani Joe Biden aliupinga uamuzi huo na kusema kwamba yeye atasimama na Israel huku wengi wakirejelea kauli yake ya mwaka mmoja uliopita ilipotolewa waranti ya kukamatwa kwa Rais Putin wa Urusi kwa kuuita kuwa ni wa kihalali.
Marekani yenyewe sio mwanachama wa mahakama ya ICC.
Ufaransa ilisema inaunga mkono hatua hiyo ya ICC huku Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán, ambaye kwa sasa anashikilia wadhifa wa Urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya, uliishutumu mahakama hiyo "kuingilia mzozo unaoendelea kwa madhumuni ya kisiasa" na kusema nchi yake isingemkamata Netanyahu. Hungary ni nchi mwanachama wa ICC.
Soma zaidi. Urusi yaitaka Magharibi kuindolea vikwazo Afghanistan
Akizungumza katika mkutano huo rais wa mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu ICC,Tomoko Akane amesema uwezo wa mahakama hiyo upo katika shinikizo kubwa kwa sasa.
"Mahakama imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya kutaka kudhoofisha uhalali na uwezo wake wa kusimamia haki na kutambua sheria za kimataifa na haki za kimsingi kwa hatua za shuruti, vitisho, shinikizo na vitendo vya hujuma. Viongozi kadhaa waliochaguliwa wanatishiwa vikali na wanakabiliwa na hati ya kukamatwa.
Vitisho hivyo ni kutoka kwa mjumbe mmoja wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa sababu tu ya kutekeleza wajibu wao wa kimahakama kwa uaminifu na kwa kwa kuzingatia mfumo wa kisheria na sheria za kimataifa.
ICC ilianzishwa mwaka 2002 na imekuwa kimbilio la mwisho la kuwafungulia mashitaka watu waliohusika na ukatili, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari. Mahakama hiyo huanzisha kesi pale mataifa husika yasipokuwa na uwezo au kutoonyesha utayari wa kushtaki vitendo vya uhalifu kwenye maeneo yao.