1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yatangaza uchunguzi mpya dhidi ya madai ya uhalifu Kongo

15 Oktoba 2024

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC Karim Khan, amesema anaanzisha upya uchunguzi nchini Kongo unaolenga madai ya uhalifu unaofanywa katika eneo lenye migogoro la Kivu Kaskazini tangu mapema mwaka 2022.

https://p.dw.com/p/4lmoB
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC Karim Khan akiwa katika mahakama hiyo mjini The Hague mnamo Septemba 26, 2022
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC Karim KhanPicha: Peter Dejong/REUTERS

Katika taarifa, Khan amesema ghasia za hivi karibuni jimboni Kivu Kaskazini zinahusishwa na matukio ya vurugu na uhasama ambayo yamekumba eneo hilo tangu katikati mwa mwaka 2002. Kutokana na hilo, tuhuma za hivi karibuni zaidi zinaangukia kwenye uchunguzi unaoendelea.

Khan asema uchunguzi Kivu Kaskazini hautakuwa wa upendeleo

Khan amesema uchunguzi wake huko Kivu Kaskazini hautahusisha vyama ama wanachama wa makundi maalumu lakini badala yake, ofisi yake itachunguza kiujumla, kwa njia huru, na bila upendeleo wahusika wote wanaodaiwa kufanya uhalifu ndani ya mamlaka ya mahakama hiyo.

Wakimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi ya Rhoe mkoani Ituri nchini Kongo wakiletewa msaada wa maji na lori la Umoja wa Mataifa mnamo Aprili 19, 2023
Wakimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi ya Rhoe mkoani Ituri nchini KongoPicha: Paul Lorgerie/REUTERS

Uamuzi huo pia unafuatia rufaa ya pili kutoka kwa serikali ya Kongo mnamo Mei 2023, ambayo iliomba uchunguzi katika kile ambacho nchi hiyo iliutaja kuwa uporaji wa kimfumo wa raslimali zake asili masharikimwa Kongo kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na kundi la waasi la M23.

Awali waasi watatu walitiwa hatiani na Mahakama ya ICC

Awali, mahakama hiyo ya ICC iliwatia hatiani waasi watatu kwa uhalifu katika mkoa wa Ituri, kaskazini mwa Kongo ikiwa ni pamoja na mbabe maarufu wa vita  Bosco Ntaganda, anayejulikana kama "The Terminator" ambaye alipatikana na hatia ya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na utumwa wa ngono.