kunahitajika usaidizi mkubwa sana wa kiutu
22 Machi 2019Katibu mkuu wa shirika la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu Ulimwenguni Elhadj As Sy alisema kadiri siku zinavyosonga idadi ya waliouawa inaweza kupindukia elfu moja, kiwango alichokisia rais wa Msumbiji Filipe Nyusi wiki jana .
As Sy aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba kando na wasiwasi juu ya idadi ya watu waliofariki kunahitajika usaidizi mkubwa sana wa kiutu kwa sababu misaada iliyofika ni kidogo ikilinganishwa na maafa makubwa yaliyoosababishwa na kimbunga hicho.
Hali katika mji wa Beira imekuwa mbaya sana kutokana na manusura kukosa chakula, maji na mahitaji mengine ya kimsingi huku kukiwa na hofu ya kuzuka maradhi yanayosababishwa na maji machafu.
Baada ya kutembelea kambi za manusura As Sy alisema hali ni mbaya sana na katika shule moja iliyo na madarasa 15 kuna manusura elfu tatu na vyoo walivyonavyo ni sita tu, anasema kilichomsikitisha zaidi ni watoto wengi waliokosa wazazi kwa kupoteana nao katika vurumai ama wazazi kufariki kutokana na mafuriko.
Mkuu wa oparesheni ya waokoaji ya Rescue South Africa, Connoe Hartnady alisema chakula zaidi kinahitajika mjini Beira.
Waziri wa ardhi na mazingira wa Msumbiji Celso Correia alisema kiasi cha watu elfu kumi na tatu hawajulikani walipo.
Zimbawe yarudi katika hali ya kawaida
Dhoruba ya kimbunga hicho ilisababisha kuvunjika kwa kingo za mito Buzi na Pungwe inayoelekea katika mji wa Beira.
Barabara katika mji huo zilizibwa, umeme kupotea na miti kutapakaa katika mji huo uliokuwa na wakazi zaidi ya 500,000.
Kimbuga Idai pia kiliathiri taifa la Zimbamwe na Malawi na kusababisha maafa. Kiasi cha watu 142 walifariki Zimbambwe na 56 nchini Malawi.
Hali nchini Zimbambwe imeanza kuwa ya kawaida baada ya barabara kufunguliwa na mawasiliano kurejeshwa.
Zipo simulizi za maafa mbali ambalo, zikiwemo za mama mmoja aliyezikwa katika kaburi moja na mwanaye, mkuu wa shule aliyesombwa na mafuriko pamoja na wanafunzi wake, wachimbaji haramu waliokumbwa na mafuriko migodini, na polisi waliosombwa na mafuriko hayo pamoja na wafungwa waliokuwa wakiwasimamia.
(RTRE/APE)