Idadi ya wanahabari waliofungwa jela Afrika iliongezeka 2021
22 Desemba 2021Ukosefu wa utulivu wa kisiasa mfano mapinduzi yaliyofanyika 2021 Sudan, Mali, Guinea na Chad- yamechangia hali ya waandishi Habari kukandamizwa au kubanwa.
Katika ripoti yake kuhusu madhila dhidi ya waandishi wa habari, ambayo ilitolewa mwezi huu wa Disemba, shirika la waandishi wa Habari wasiokuwa na Mipaka RSF, ilitoa tahadhari kuhusu ongezeko la waandishi wanaofungwa jela ulimwenguni kote.
RSF inasema waandishi wa Habari wanalengwa na serikali au makundi yenye silaha yanayotaka kudhibiti taarifa kwa wananchi, hasa katika maeneo yanayokumbwa na machafuko mfano Cameroon, ukanda wa sahel, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia na Somalia.
Hatari kwa waandishi habari Afrika Mashariki
Arnaud Froger ambaye ni mkuu wa RSF barani Afrika amesema ukanda wa Afrika Mashariki ndio hatari zaidi kwa waandishi wa habari barani Afrika.
"Zaidi ya wanahabari 100 walikamatwa kiholela, 26 wakafungwa mwaka huu. visa vingi vilitokea, Cameroon, Nigeria, Eritrea, Benin, Rwanda, Ethiopia, Uganda na Sudan," amesema Froger.
CPJ: Idadi ya waandishi waliofungwa duniani yaongezeka
Kwa mfano nchini Eritrea, rais wa nchi hiyo Isaias Afwerki alipiga marufuku vyombo vyote vya habari huru mwaka 2001 na nchini Djiubouti, hakuna uhuru wa vyombo vya habari hivyo kufanya mataifa hayo kuwa kama jangwa linapokuja suala la upatikanaji habari.
Kulingana na faharasa ya Uhuru wa habari mwaka 2021, Eritrea iliorodheshwa nafasi ya mwisho ulimwenguni kote.
Nchi tatu ambazo ziliwafunga jela waandishi wa habari wengi mwaka 2021barani Afrika kuliko nyingine zote ni Eritrea, Ethiopia na Rwanda. Zote ziko katika ukanda wa Afrika mashariki.
Kubanwa kwa uhuru wa vyombo vya habari Ethiopia
Mwezi uliopita, Ethiopia ilikosolewa Zaidi na mashirika ya kutetea haki za binadamu na pia Umoja wa Mataifa kwa kubana uhuru wa vyombo vya habari wakati vita kati ya jeshi la shirikisho na vikosi vya Tigray na Oromo vikiendelea.
Siku ya Kimataifa ya kukomesha uhalifu dhidi ya wanahabari
Wiki iliyopita, wanahabari watatu walishtakiwa mahakamani Ethiopia kwa madai ya kukuza ugaidi, baada ya kuwahoji wanamgambo wa Oromo, ambao Ethiopia chini ya serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed, imewataja kama kundi la kigaidi
Froger ameliambia shirika hili (DW) kwamba kile ambacho wanahabari wanaweza kuripoti ni takwimu rasmi za serikali na kauli za serikali.
Somalia ambayo pia iko katika ukanda wa Afrika Mashariki pia imetajwa kama mojawapo ya nchi hatari Zaidi barani Afrika kwa waandishi wa habari.
Uganda yawafunga jela askari waliowapiga wanahabari
Mwaka huu pekee wanahabari wawili wameshauwa, hivyo kuongeza idadi ya wanahabari ambao wameuawa nchini humo tangu mwaka 2010 kupita 50. Akizungumza na DW kuhusu mazingira ya kazi kwa wanahabari nchini Somalia, Omar Faruk ambaye ni mwenyekiti wa chama cha waandishi habari nchini Somalia amesema:
"Mazingira ya Somalia huwa magumu sana kwa wanahabari kufanya kazi kwa sababu ya vitisho kwa usalama wao. Na usalama hapa si tu dhidi ya machafuko lakini pia usalama wa kisheria. Wanahabari nchini Somalia hushambuliwa mara kwa mara na maafisa, kukamatwa kiholela au hata kupelekwa kortini".
Aidha, Somalia pia ina sifa mbaya ulimwenguni kote katika kusuluhisha masuala ya mauaji ya wanahabari. Hayo ni kulingana na faharasa iliyotolewa na Kamati ya kuwalinda waandishi wa habari mwaka 2021.
Sifa nzuri ya Ghana yadidimia
Polisi Tanzania yashutumiwa kwa kuhangaisha wanahabari
Baadhi ya nchi za Afrika zilizokuwa na sifa nzuri kuhusu uhuru wa habari mathalan Ghana zimeanza kupoteza sifa hizo.
Kulingana na faharasa ya mwaka huu, Ghana ilishuka hadi nambari 30 kutoka nambari 22 mwaka 2015, huku kukiwa na ongezeko la ripoti ya visa vya wanahabari kuteswa na haki zao kukiukwa mikononi mwa maafisa wa usalama.
(DW)