1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wanaohitaji chakula Kenya yaongezeka

Yusra Buwayhid
14 Agosti 2019

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaohitaji chakula inaongezeka na hadi sasa imefika hadi milioni 2.6. Utapiamlo pia ni tatizo miongoni mwa watoto na wanawake wajawazito.

https://p.dw.com/p/3Ntfn
Kenia Dadaab-Flüchtlingslager USA Aid
Picha: Getty Images/AFP/P. Moore

Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula nchini Kenya, imeongezeka kutoka milioni 1.1 mwezi Februari hadi watu milioni 2.6 mwezi wa Agosti. Na zaidi ya watoto laki 357 na wanawake wajawazito wanakabiliana na makali ya utapiamlo.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa mamlaka ya kitaifa inayohusika na kukabiliana na ukame, ambayo imeonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi kufikia mwezi Septemba iwapo mikakati haitawekwa kukabili hali hiyo.

Mavuno duni katika msimu uliopita na ukosefu wa mvua ya kutosha vimechangia kuzorota kwa hali ya usalama wa chakula nchini Kenya.

Idadi kubwa ya watu walioathirika zaidi wapo kwenye kaunti kumi za Turkana, Mandera, Garissa, Wajir, Marsabit, Baringo, Tana River, Kitui, Makueni na Kilifi.

Utafiti wa shirika la umoja wa mataifa la UNICEF unaonyesha kuwa takriban watoto laki 175 katika maeneo haya wameshindwa kuhudhuria msomo kufuatia makali ya ukame.