1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

IGP Kenya ajiwajibisha kwa vifo vya waandamanaji

12 Julai 2024

Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kenya Japhet Koome amejiuzulu kufuatia ukosoaji mkali baada ya maandamano ya kuipinga serikali kusababisha vifo kadhaa. Rais William Ruto amemteua naibu wa Koome kukaimu nafasi hiyo.

https://p.dw.com/p/4iEmy
Kenya aliekuwa mkuu wa jeshi la polisi, Japhet Koome
IGP Japhet Koome alikosolewa na Rais Ruto kwa kuwa kiongozi dhaifu zaidi akimshtumu kushindwa kudhibiti maandamano ya vijana wa Gen-Z.Picha: AP Photo/picture alliance

Hatua hiyo imejiri siku moja baada ya Rais William Ruto kulifuta kazi takriban baraza lake lote la mawaziri, katika juhudi za kutuliza hasira za umma dhidi ya serikali yake baada ya maandamano yalioanza kwa amani kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi kugeuka ghasia.

Ofisi ya rais ilisema kwenye taarifa kuwa Ruto "amekubali kujiuzulu" kwa inspekta jenerali mkuu wa polisi, IGP Japhet Koome, ambaye amehudumu katika wadhifa huo tangu Novemba 2022.

Baadhi ya vijana wa Gen-Z waliokuwa nyuma ya maandamano hayo walikuwa wamemtaka Koome aondoke, huku polisi wakituhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano hayo, ambayo yamegeuka kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa urais wa Ruto wa takriban miaka miwili.

Ruto amechukua hatua kadhaa kuwatuliza waandamanaji, ikiwa ni pamoja na kuachana na mswada wa fedha uliohusisha ongezeko la kodi ambalo halikupendeza wengi.

Kenya | Maandamano Nairobi
Polisi wa Kenya walishtumiwa kutumia nguvu iliyopitliza na kusababisha vifo vya waandamanaji. Sasa lawama hizo zimemgharimu mkuu wao Japhet Koome nafasi yake.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Mnamo siku ya Alhamisi, Rais Ruto aliwafuta kazi mwanasheria mkuu na mawaziri wote wa baraza la mawaziri, isipokuwa waziri kiongozi anaeshughulikia pia mashauri ya kigeni Musalia Mudavadi na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

'Hatuwezi kumuamini tena'     

Lakini tangazo hilo la kuvunjwa kwa baraza la mawaziri, licha ya kukaribishwa na baadhi ya watu, halikuwafurahisha baadhi ya vijana wa Kenya waliovunjwa moyo na kushindwa kwa Ruto kutimiza ahadi zake za uchaguzi wa 2022, kuhusu kubuni nafasi za kazi na kukuza utajiri wao.

Soma pia: Rais wa Kenya avunja baraza lake la mawaziri baada ya wiki kadhaa za maandamano

"Tutarejea mtaani hadi Ruto aondoke. Amepoteza miaka miwili madarakani akisafiri na kusema uwongo," alisema Hyrence Mwangi, mwenye umri wa miaka 25.

Maandamano hayo yalioanza kwa amani, yalichafuka baada ya polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji waliovamia bunge mnamo Juni 25, na kupora jengo hilo ambalo liliwashwa moto kwa upande mmoja.

Kenya Nairobi  Rais William Ruto
Rais William Ruto ametangaza hatua kadhaa kutuliza hali nchini mwake, ikiwa ni pamoja na kulifuta kazi karibu baraza lake lote la mawaziri.Picha: TONY KARUMBA/AFP

Wakati maandamano makubwa ya mitaani yamepungua, hasira dhidi ya serikali hazijapungua, hasa dhidi ya polisi, huku mashirika ya kutetea haki yakisema watu 39 waliuawa katika maandamano hayo.

"Tulipoenda mitaani mara ya kwanza, Ruto alitupuuza kama kundi la wahuni na wahalifu waliokodiwa, kisha akaja baadaye na kuanza kusema atafanya mabadiliko," alisema Jackson Rotich mwenye umri wa miaka 27.

"Hatuwezi kumuamini."

Mtaalamu wa TEHAMA Cyrus Otieno, 27, alikuwa miongoni mwa waliokuwa wamemtaka Koome aondolewe, akisema "lazima ashtakiwe kwa ukatili wa polisi".

Mwanafunzi wa sheria Melisa Agufana, 24, alikaribisha kuvunjwa kwa baraza la mawaziri, akisema alitaka "kumshukuru rais kwa kusikiliza".

Soma pia: Rais William Ruto wa Kenya aahidi mabadiliko baada ya maandamano

Aliongeza kuwa mawaziri "wamepoteza miaka miwili bila kufanya lolote isipokuwa kuzunguka tu wakipeperusha bendera yetu ya taifa."

Mwanzo mpya wenye changamoto lukuki

Wachambuzi wamesema hatua hiyo imeweka uwezekano wa kuanza upya, lakini walionya juu ya hatari zaidi.

"Changamoto ambayo Ruto anakabiliwa nayo sasa ni kuunda baraza jipya la mawaziri ambalo linajumuisha maslahi mbalimbali, wakati huo huo kutuliza hasira za wananchi mbele ya vuguvugu lisilo na kiongozi," Gabrielle Lynch, profesa wa siasa linganishi katika Chuo Kikuu cha Warwick, aliiambia AFP.

Hofu ya vijana kutekwa wakati wa maandamano ya Kenya

Wiki iliyopita, Ruto alitangaza kupunguza kupunguza pakubwa matumizi ya serikali, ikiwa ni pamoja na gharama za usafiri na ukarabati, na kusema ataongeza mikopo ili kulipia baadhi ya huduma hata wakati Kenya inakabiliana na deni kubwa la nje linalokaribia asilimia 70 ya Pato la Taifa.

Soma pai: Mabomu ya machozi, mawe, moto Wakenya wakimkaidi Ruto

Mgogoro huo ulisababisha kampuni ya Moody's yenye makao yake Marekani kushusha zaidi kiwango cha ukopeshekaji wa Kenya, ikionya juu ya mtazamo hasi, ambao utafanya ukopaji kuwa ghali zaidi kwa serikali hiyo inayokabiliwa na ukata mkubwa.

Ruto alisema Alhamisi kwamba "atashiriki mara moja katika mashauriano ya kina na sekta mbalimbali na mirengo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali yenye msingi mpana", bila kufafanua zaidi.

Chanzo: Mashirika