Usawa wa jinsia na nguvu kazi
24 Februari 2015Katika nchi nyingi kuna pingamizi chungu nzima za kisheria zinazowazuwia akinamama kuwajibika kiuchumi" amesema Lagarde katika blogi yake.
Katika ulimwengu unaokuwa,wanawake wanaweza kusaidia ikiwa watapatiwa nafasi ya kuwajibika badala ya kufanyiwa njama zenye madhara."
Christine Lagarde,mwanamke wa kwanza kuongoza shirika la fedha la kimataifa,ameipatia sura mpya taasisi hiyo ya fedha na kuimarisha nafasi ya wanawake katika uchumi wa dunia akihoji kwa kufaya hivyo matumaini ya ukuaji wa kiuchumi yanaongezeka na kuimarisha maendeleo.
Hoja hizo zinaweza kushawishi mengi katika wakati huu ambapo ukuaji jumla wa kiuchumi unapungua na katika nchi ambako wakaazi wake wanazeeka haraka mfano wa Japan ambako kiwango cha nguvu kazi ya akinamama kiko nyuma ya kile cha jumuiya ya OECD.
Lakini shirika la fedha la kimataifa IMF linabidi kufuata msimamo wa tahadhari katika suala hili na kuepuka kukosoa kwa uwazi kabisa sheria katika nchi 188 wanachama,ikiwa ni pamoja na nchi mfano wa Mali na Yemen ambazo ni miongoni mwa nchi zinazoburura mkia katika juhudi za kuleta usawa wa jinsia.
Usawa wa jinsia utasaidia kuimrisha ukuaji wa kiuchumi
Shirika la fedha la kimataifa lilitaka kulenga hoja zake kiuchumi na kusema katika utafiti wake uliopita kwamba ikiwa idadi ya nguvu kazi ya kike italingana na ile ya wanaume,hali hiyo inaweza kuimrisha ukuaji wa kiuchumi kwa asili mia tano nchini Marekani ,asili mia 9 nchini Japan na asili mia 34 nchini Misri.
Katika utafiti uliofanywa na shirika la IMF na kuchapishwa jumatatu iliyopita,watumishi wa shirika hilo la Umoja wa mtaifa wamegundua kwamba licha ya maendeleo katika suala la kuleta usawa wa jinsia,takriban asili mia 90 ya nchi bado zina angalao sheria moja inayoleta pingamizi katika suala la usawa wa jinsia na katika nchi nyengine 20 kuna sheria kama kumi au zaidi kama hizo.
Sheria hizo ni pamoja na vizuwizi katika haki za akinamama kumiliki rasli mali na zile zinazowaruhusu wanaume kuwazuwia wake zao kwenda kufanya kazi au kuwazuwia akinamama kufanya aina fulani ya kazi.
Mwamko katika jamii umerahisisha mabadiliko
Uchunguzi huo umegundua kwamba sheria zilizofanyiwa marekebisho zinazowabagua akinamama zina mafungamano na kuzidi idadi ya akinamama wanaofanyakazi ingawa uchunguzi huo unakiri marekebisho ya sheria huenda yamesababishwa na mtazamo wa aina mpya katika jamii.
Wataalamu wa IMF wamesema."Kwa kushauri fursa sawa....uchunguzi huu haujalenga kuingilia katika masuala ya utamaduni na dini katika nchi husika"
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman