IMF yaidhinisha mkopo wa dola milioni 368 kuisaidia DRC
17 Desemba 2019Shirika la fedha duniani IMF limeidhinisha mkopo wa Dola milioni 368.4 kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ili kuwezesha nchi hiyo kukidhi mahitaji ya haraka. IMF imesema mazingira ya kiuchumi bado ni magumu na yanaweza kusababisha uchumi kuyumba.
Kwenye taarifa yake IMF, imesema ukuaji halisi wa pato la taifa unakadiriwa kushuka kwa asilimia 4.5 mwaka huu wa 2019 kutoka asilimia 5.8 ya mwaka 2018, huku fedha ya kigeni ikipungua kiwango cha chini.
Rais Felix Tshisekedi aliyeingia madarakani Januari mwaka huu, ameahidi kuleta mageuzi na kupambana na ufisadi katika taifa hilo maskini lakini lenye utajiri mkubwa wa madini barani Afrika.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inashikilia nafasi ya 161 kati ya 180 kwenye orodha ya ufisadi iliyotolewa mwanzoni mwa mwaka huu.
IMF imesema serikali mpya imejizatiti kushughulikia masuala yote yanayohusiana na utawala mbovu, mazingira yasiyoridhisha kufanya biashara na umaskini ulioenea.