1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya fedha duniani yaonya dhidi ya sera za Marekani

Shisia Wasilwa
12 Juni 2018

Shirika la fedha ulimwenguni IMF, Shirika la Biashara duniani -WTO yameonya kuwa sera za Marekani za kujilinda kibiashara zinaweza kuwa na athari kwa uchumi wa dunia,kwenye mkutano uliofanyika mjini Berlin, Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2zLZQ
Deutschland Treffen Angela Merkel & internationale Finanz-Chefs
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Onyo hilo lilitolewa katika mkutano uliotishwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wa mashirika kadhaa ya kimataifa.

Merkel, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa nchi waliohudhuria mkutano wa nchi saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani  G-7 nchini Canada wiki iliyopita, alisema kuwa wale waliokuwa kwenye mkutano huo, walishawishika kuwa, maendeleo endelevu ya uchumi ulimwenguni yanaweza kuafikiwa kupitia ushirikiano.

Aliongeza kusema kuwa, uamuzi wa utawala wa Trump wa kutoza ushuru mpya wa bidhaa za chuma cha pua na bati uko kwenye hatua ngumu na yenye utata.

Mkutano waitishwa na Merkel

Mkutano huo uliwajumuisha viongozi wa Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF, Shirika la Bishara dunia WTO, Shirika la Ustawi wa Kiuchumi na Maendeleo, Benki ya Maendeleo  ya Afrika pamoja na Shirika la Kazi Duniani ILO.

Mkutano kati ya viongozi wa mashirika ya fedha na kansela Merkel
Mkutano kati ya viongozi wa mashirika ya fedha na kansela Merkel Picha: Reuters/M. Sohn

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la IMF Christine Lagarde aliwaambia waandishi habari, "uchumi wa dunia ulikuwa mzuri na kwamba kuna matumani kila siku."

Merkel na  Lagarde,wamesema kuwa uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.9 mwaka huu, lakini huenda sera za Marekani za kulinda bidhaa zake zikahujumu ukuaji huo.

Kufuatia mkutano wa kimataifa yenye uwezo mkubwa ulimwenguni wa G-7 nchini Canada , awali Trump alikubali kuunga mkono taarifa ya kuhusu biashara ambayo ingetolewa na viongozi wengine. Lakini Rais huyo wa Marekani baadaye alijiondoa, kwa kudai kuwa alikuwa ametengwa na Waziri mkuu wa Canada.

Sera ya Marekani kuhujumu uchumi wa ulimwengu

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May alimpongeza waziri mkuu wa Canada kwa uongozi wake wa kusimamia mkutano huo kwa kile alichokitaja, "mkutano mgumu uliokuwa na mazungumzo ya wazi."

Viongozi wa mataifa ya G-7
Viongozi wa mataifa ya G-7Picha: Getty Images/M.Medina

May alielezea wasiwasi wake na masikitiko kufuatia hatua ya Marekani ya kutoza ushuru bidhaa za chuma cha pua na bati na kupendekeza kufanyika kwa mazungumzo ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Rais wa Halmashauri kuu ya  Ulaya Jean Claude Juncker, pia ametoa kauli ya kumuunga mkono Waziri Mkuu wa Canada Trudeau, ambaye alishambuliwa na Rais Trump na maafisa wake, "wakimuita mtu dhaifu na asiye na uaminifu."

Trump aliwakosoa washirika wake kwenye mtandao wa Twitter kwa kusema kuwa Marekani imevumilia kwa miongo mingi biashara inayoegemea upande mmoja.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp, Dpa,

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman