IMF: Ukuaji wa chumi za Mashariki ya Kati kushuka 2024
11 Februari 2024Mkuu wa shirika hilo la IMF Kristalina Georgieva, ameliambia Jukwaa la Sera za Uchumi kwa mataifa ya kiarabu linalofanyika mjini Dubai kwamba licha ya hali zisizotabirika,uchumi wa dunia umesalia kuwa himilivu, huku akionya kuhusu uwezekano wa athari kubwa zaidi kwa chumi za kanda ya Mashariki ya Kati kutokana na mzozo unaoendelea katika Ukanda huo wa Gaza.
Chumi zinazopakana na Israel na maeneo ya Palestina zashuhudia athari za mzozo wa Gaza
Georgieva amesema, chumi za mataifa yanayopakana na Israeli na maeneo ya Palestina zimeshuhudia mzozo huo ukiathiri mapato yanayotokana na utalii huku mashambulizi katika Bahari ya Shamu yakiathiri gharama za usafirishaji mizigo kimataifa.
Soma pia:IMF: Ukuaji uchumi duniani kushuka kwa 3% mwaka 2023
Georgieva, ameliambia jukwaa hilo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa wakuu wa serikali duniani mjini Dubai kwamba masuala hayo yameongezea changamoto za chumi ambazo bado zinafufuka kutokana na misukosuko ya awali.