1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Imran Khan aachiwa kwa dhamana

12 Mei 2023

Mahakama ya nchini Pakistan imeagiza aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Imran Khan kuachiwa kwa dhamana kwa wiki mbili, baada ya kukamatwa kwa madai ya ufisadi, hatua iliyoibua maandamano na ghasia kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/4RH17
Pakistans ehemaliger Premierminister Imran Khan
Picha: imago images/Russian Look

Wafuasi wa chama cha Imran Khan cha Tehreek-E-Insaf waliokuwa nje ya jengo la mahakama walishangilia uamuzi huo na kusema wana imani kwamba maamuzi kama hayo yatalipeleka taifa hilo kwenye mazingira mazuri.

Soma Zaidi: Pakistan yazizima baada ya kukamatwa kwa Imran Khan

Mahakama Kuu ya Islamabad imemuachia Khan kwa dhamana kwa wiki mbili, na kuiagiza taasisi ya kupambana na ufisadi kutomkamata Khan katika kipindi hicho, hii ikiwa ni kulingana na wakili wake Faisal Chaudhry, alipozungumza na shirika la habari la Reuters.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliingia mahakamani mapema hii leo akiwa amezungukwa na mawakili na wanajeshi wa usalama. Nje ya jengo la mahakama, wafuasi wake walikuwa wakipambana na polisi katika maeneo mbalimbali katika mji mkuu, Islamabad, vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti.

Pakistan I Baadhi ya waandamanaji wakiwa wamewasha moto na kuzuia barabara wakishinikiza kiongozi wao Imran Khan kuachiwa huru.
Kuakamatwa kwa aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan kuliibua maandamano na machafuko kote nchini humo.Picha: Asif Hassan/AFP

Baada ya agizo hilo la mahakama kutangazwa, waziri wa mambo ya ndani Rana Sanaullah alisema tayari ameyaagiza majeshi ya usalama kuheshimu maagizo ya mahakama na hawataki kusikia ukiukwaji wa aina yoyote.

Mwenyewe Imran Khan alizungumza baada ya uamuzi huo wa mahakama alisema mahakama kuu haikuwa na sababu yoyote ya kumkamata.

"Nilikuwa ndani ya Mahakama Kuu, hawakuwa na uhalali wa kunikamata, waliniteka. Walinionyesha hati ya kukamatwa mara ya kwanza nikiwa jela, hili linatokea kwenye sheria ya msituni. Wanajeshi waliniteka..... Polisi walikuwa wapi?... Wako wapi?... sheria? ni sheria ya msituni!!!. Inaonekana, kuna sheria ya kijeshi iliyotangazwa hapa. Watu 40 waliuawa, nilisikia mara ya kwanza, nilipokwenda mahakama ya Juu," alilalama Khan.

Soma Zaidi:Pakistan: Polisi wamfungulia Imran Khan mashtaka ya ugadi na mengineyo.

Khan, aliyewahi kuwa championi wa kriketi na baadae kugeukia siasa alivuliwa wadhifa wa waziri mkuu Aprili mwaka uliopita, baada ya kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye. Kulingana na uchunguzi wa maoni, kiongozi huyo bado ni mashuhuri zaidi nchini Pakistan.

Hapo jana mahakama ya juu zaidi iliamua kiongozi huyo kuachiliwa huru, hatua iliyorejesha utulivu, baada ya taifa hilo kushuhudia makabiliano kati ya wafuasi wa Imran Khan na vikosi vya usalama tangu kiongozi huyo alipokamatwa kwa madai ya ufisadi.