India: Modi kuapishwa pamoja na washirika wa muungano
9 Juni 2024Huku Modi akiwa bado hajatangaza baraza lake la mawaziri, hafla ya kiapo katika kasri la rais baadae Jumapili itafuatiliwa kwa karibu wakati maafisa 30 wanaotarajiwa kuwa mawaziri pia watakula kiapo cha kuheshimu katiba.
Soma pia: Mpinzani wa Modi ateuliwa kuongoza kambi ya upinzani bungeni
Chama cha Modi cha siasa kali za kizalendo - Bharatiya Janata - BJP kiliongoza nchi kwa muongo uliopita lakini mara hii kimeshindwa kupata matokeo ya kishindo kama ilivyokuwa katika chaguzi mbili za nyuma. Modi alilazimika kufanya mazungumzo ya haraka na muungano wenye vyama 15 wanachama, wa National Democratic Alliance, ambao ulimhakikishia idadi ya viti anavyohitaji bungeni ili kuunda serikali.
Vyama vikubwa vya miungano vimetoa masharti ya kupewa nyadhifa kubwa ili navyo vikubali kumuunga mkono. Inaripotiwa kuwa chama cha Telgu Desam - TDP, mshirika mkubwa kabisa wa BJP na viti 16, kitapata nyadhifa nne za uwaziri. Chama kikubwa kinachofuata, Janata Dal na viti 12, kitapewa mawaziri wawili. Baraza la mawaziri lililopita la Modi lilikuwa na mawaziri 81.