India na Pakistan zapimana nguvu Kashmir
1 Machi 2019Ingawa ahadi ya Pakistan ya kumuachia huru rubani wa ndege ya India imepunguza kitisho cha kuenea mzozo huo, hata hivyo mizinga haijasita bado katika eneo hilo la milima ya Himalaya lililogawika tangu mwaka 1947 kati ya majirani hao wawili.
Mzozo huo umezidi makali wiki hii pale ndege za kivita za nchi hizo mbili hasimu zilipoingia katika eneo la adui kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa na kupelekea jumuia ya kimataifa kuhofia mzozo huo utazidi makali.
India na Pakistan kila mmoja anadai haki ya kumiliki eneo hilo la milima wanakoishi jamii kubwa ya waislam. Nchi hizo mbili zimeshateremka vitani mara mbili kwaajili hiiyo.
Rubani aachiwa kwasababu za kiutu
Pakistan inapanga kumuachia huru rubani wa India aliyekamatwa kufuatia mapigano ya wiki hii. Luteni kanali Abhinandan Varthaman ataachiwa huru katika eneo la mpakani la Wagah lililoko kati ya mji wa Pakistan wa Lahore na ule wa Amristar nchini India. Maelfu ya watu wamekusanyika upande wa India kumpokea yule wanaemtaja kuwa shujaa. Akitangaza uamuzi huo waziri mkuu wa Pakistan, Imran Khan amesema hiyo ni ishara ya amani kuelekea India. Nae wakili Shiraz Anjum anashadidia kutokana na "Sababu za kiutu na kulingana na makubaliano ya Geneva, Pakistan haiwezi kuendelea kumshikilia rubani huyo wa India. Anabidi akabidhiwe serikali ya India wakati wowote ule. Sisi wapakistan tunaharakisha ili tuuonyeshe ulimwengu tunaheshimu utu."
Upinzani nchini India unataka kujua kama opereshini imefana
Viongozi wa dunia wamekuwa wakiwahimiza viongozi wa nchi hizo mbili wajizuwie baada ya mzozo huo kuzidi makali kufuatia shambulio la bomu lililoangamiza maisha ya wanajeshi 40 wa India february 14 iliyopita.
Mzozo huu mpya unatokea wakati mgumu kwa waziri mkuu wa India Narendra Modi anaekabiliwa na uchaguzi mkuu unaobidi uitishwe mwezi may unaokuja. Upande wa upinzani unataka upatiwe maelezo kwa umbali gani opereshini ya kijeshi ya ndege za India zimefana huko Kashmir.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu