1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yakumbwa na janga kubwa la kibinaadamu kutokana na mafuriko

Gregoire Nijimbere29 Julai 2005

Nchi ya India imekabiliwa na janga kubwa la kibinaadamu kufuatia mafuriko makubwa katika jimbo la Maharashtra ambako unapatikana mji mkuu wa kibiashara wa Bombay. Watu takriban 900 wameshakufa pamoja na maelfu ya mifugo. Inahofiwa kuwa maradhi ya kuambukiza yanaweza kutokea na hivyo kusababisha maafa zaidi.

https://p.dw.com/p/CHfd
Picha ya sehemu moja ya Bombay
Picha ya sehemu moja ya BombayPicha: AP

Idadi ya wahanga wa mafuriko hayo katika jimbo zima la Maharashtra na mji wa Bombay imezidi sasa watu 800, kulingana na mkuu wa polisi katika mji muhimu kiuchumi wa Bombay Bwana Roy.

Idadi ya awali ya watu 786, imeongezeka leo hii baada ya kupatikana maiti zingine karibu na mji wa Bombay. Katika mji huo pekee, watu 370 walifariki dunia. Watu wengine wapatao 513 waliuawa katika sehemu za vijijini za jimbo hilo la Maharashtra.

Wahanga wengi wa mafuriko hayo, aidha walikufa kwa kuzama katika mito, au kwa kufunikwa na mmomonyoko wa ardhi au mporomoko wa majumba.

Leo katika tukio la wasi wasi, watu watano wameuawa na wengine 18 wamejeruhiwa kwa kukanyagwa katika msongamano mkubwa wa watu waliyokuwa wakikimbia kujisalimisha, baada ya kuenea uvumi kwamba kizuwizi cha mwambao wa mto kimezidiwa na maji kufurika.

Hayo yametokea katika kitongoji cha mji wa Bombay cha Nehru Nagar.

Siyo tu wanaadamu ambao wameangamia katika mafuriko hayo. Bali pia mifugo. Kulingana na tarakwim za wizara ya mambo ya ndani, maiti za ng’ombe 1,034 zimeonekana kando kando na barabara katika sehemu za magharibi na mashariki za mji wa Bombay, baada ya kiwango cha mafuriko kupungua.

Mbuzi wapatao 17 elfu walikufa maji pia.

Waziri mkuu wa shirikisho la India Manmohan Singh ambae jana alizuru kwa helikopta eneo lililoathiriwa, alisema ameskitishwa na janga hilo la kibinaadamu na kaahidi msaada wa bilioni 7 za salafu ya India, sawa na milioni 162 za dola za kimarekani kwa ajili ya ukarabati.

Eneo hilo liemeathirika sana. Jumuiya ya kibiashara ya shirikisho la India, imesema kwamba hasara iliotokea, inakadiriwa kufika bilioni 10 za salafu ya taifa, ikiwa ni sawa na milioni 220 za dola za kimarekani.

Picha za eneo hilo zilizochukuliwa angani, zinaonyesha mabaki ya majumba yaliyozama katika maji na udongo na misululu mirefu ya magari katika sehemu za milimani.

Serikali ya kijimbo ambayo inahofia kuzuka kwa magonjwa ya kuambukiza, imeitisha mkutano wa dharura wa vyama vyote vya kisiasa kwa ajili ya mpango wa kurejesha hali ya kawaida.

Afisa wa serikali Srikant Singh, amesema kuwa wataanzisha hivi punde operesheni kabambe ya kuusafisha mji.

Nvua hizo ambazo zilianza kupiga juzi jumatano, zilifikia hadi kiwango cha mita moja kwa siku na hivyo kuvunja rikodi mbaya ya mwaka wa 1910. Mifereji ya maji machafu iliziba na kuharibu vibaya mazingira. Katika mitaa kadhaa, wakaazi hawana maji safi. Miti ya waya za umeme ilianguka kutokana na upepu mkali ulioambatana na nvua hizo.

Leo imearifiwa kuwa nvua zimepungua. Shughuli za uchukuzi zimeanza taratibu na watu wameanza kutembea katika sehemu fulani ambako kiwango cha maji barabarani kimeshuka. Uwanja wa ndege umefunguliwa tena pamoja na baadhi ya benki na shule.

Lakini athari bado kutoweka kabisa. Idara ya udadisi wa hali ya hewa, imetabiri uwezekano wa kunyesha nvua zingine katika jimbo hilo la Maharashtra na mji wake mkuu Bombay wenye wakaazi milioni 15.