India yataka biashara zaidi na Afrika
30 Oktoba 2015Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali 41 kutoka Afrika walihudhuria mkutano huo wa kilele uliofanyika kwa mara ya tatu uliozingatiwa kuwa hatua kamambe ya kidiplomasia yenye lengo la kulivutia bara la Afrika lenye utajiri mkubwa wa malighafi.
Waziri Mkuu wa India aliwaambia viongozi wa Afrika kwamba ni heshima kubwa kwa India kuwa mshirika wa maendeleo wa Afrika. Amesema ushirikiano huo unavuka malengo ya kiuchumi. Msaada wa maendeleo uliotangazwa na India kwa nchi za Afrika unajumuisha fursa za elimu 50,000 kwa ajili ya wanafunzi wa Afrika.
India pia itatoa,kwa nchi za Afrika mkopo wa jumla ya dola Bilioni 10 wenye masharti nafuu sambamba na mpango wa maendeleo wa dola Bilioni 7.4 unaotekelezwa sasa. Mikopo hiyo itatolewa kwa riba za chini ya viwango vya kawaida. Mabara ya India na Afrika pia yataimarisha uhusiano wa kibiashara na nishati.
Biashara kati ya mabara hayo imeongezeka mara mbili na kufikia thamani ya karibu dola Bilioni 72 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Akiufunga mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika na India,Waziri Mkuu Narendra Modi amesema nchi yake itaweka kipaumbele katika juhudi za kuongeza biashara na vitega uchumi barani Afrika.
Waziri Mkuu Modi amesema India itaifanya biashara baina yake na Afrika kuwa linganifu. Kampuni za India zinawania kupata masoko barani Afrika wakati nchi za Afrika zinataka kunufaika na tajiriba ya India katika tekinolojia ya habari na mawasiliano. Modi ameeleza kwamba nishati kutoka Afrika ndiyo inayoindesha injini ya uchumi wa India.
Afrika yataka heshima kwenye Umoja wa Mataifa
Kwenye mkutano wao mjini New Delhi viongozi wa Afrika na India pia walisisitiza umuhimu wa mabara yao kuwa na viti vya kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akihutubia kwenye mkutano wa mjini New Delhi ,Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambae pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, alisema kwamba mabara ya Afrika na India yamekuwa yanazingatiwa kama wanachama wa daraja la chini kwenye Umoja wa Mataifa.
Mugabe amesema, kweli haki za Afrika na India zinapaswa kuheshimiwa hasa kutokana na ukweli kwamba thuluthi moja ya binadamu duniani ni Waafrika na Wahindi. Viongozi wa Afrika waliohudhuria mkutano wa kilele wa mjini New Delhi ni pamoja na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Rais Abdel Fatah al -Sisi wa Misri.
Mwandishi: Kohlman,Thomas/Mtullya Abdu.
Mhariri:Yusuf Saumu