India yapoteza watu 3,000 kwa siku kutokana na COVID-19
28 Aprili 2021Ndani ya kipindi cha masaa 24, Wizara ya Afya ya India imesajili vifo 3,293 vinavyohusiana na maambukizo ya corona, na hivyo kuifanya idadi kamili ya watu waliokwishapoteza maisha hadi sasa kufikia 201,187.
Ndani ya kipindi hicho hicho, watu wengine 362,567 wamesajiliwa kuambukizwa virusi hivyo, ikiwa ni idadi kubwa kabisa kuwahi kusajiliwa duniani kwa siku moja na ikiwa ni siku ya saba mfululizo kwa idadi kupanda kwa kasi namna hiyo.
Kwa hisabu hii, sasa India ina watu milioni 17.9 walioambukizwa virusi vya corona, ikitanguliwa na Marekani yenye milioni 32.1.
Mifumo ya afya inaripotiwa kuzidiwa nguvu na maeneo ya kuzikia watu yamelemewa.
Upungufu wa vitanda vya kulazia wagonjwa na mitungi ya gesi ya oksijini ni wa hali ya juu.
Hospitali zalemewa
Picha za vidio zinazotumwa mitandaoni zinaonesha jamaa wa wagonjwa wakipigania ndugu zao ama wakionesha hasira zao kwa ukosefu wa huduma.
"Asilimia 80 ya vifo vinatokana na utelekezwaji wa matibabu hapa. Nilichogunduwa ni kwamba tungeliweza kuwaokowa watu. Walikuwepo hospitali na hawakupata huduma muafaka waliyoihitaji kwa sababu hakuna oksijini, hakuna madawa, hakuna sindano, watu wanakufa tu hapa," alisema Nishant Wadhwan, ambaye alimpoteza ndugu yake kwenye kiunga cha Ghaziabad karibu na Uttar Pradesh.
Licha ya kwamba kwa idadi ya vifo, India iko nyuma ya Marekani, Brazil na Mexico, ambazo zote zimeshavuuka vifo 200,000 hadi sasa, wataalamu wanasema wastani wa wagonjwa wapya 300,000 na vifo 3,000 kwa siku unalipelekea taifa hilo la kusini mwa Asia kwenye kuvunja rikodi ya dunia hivi karibuni.
Msaada wa kilimwengu
Majimbo kumi ya taifa hilo la pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ulimwenguni yanayongoza kwa kuwa na asilimia 74 ya maambukizo, likiwemo Maharashtra na mji mkuu New Delhi, ambayo yote yamewekewa zuio la shughuli za kawaida.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeomba mataifa makubwa kuisaidia haraka India.
Marekani imesema itatuma mashine za kupumulia, mitungi ya gesi na vidonge vya kupambana na virusi.
Wataalamu wanasema ongezeko hili la kasi la maambukizo linatokana na kuzaliwa aina mpya ya kirusi cha corona, ambacho kimejibadilisha mara mbili zaidi ya awali, na watu kushindwa kuzingatia hatua za kujilinda.
Mataifa kadhaa yamezuwia ndege kutoka na kwenda India, yakiwemo Australia, Malaysia, Ujerumani, Ubelgiji na Italia.