1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ines Pohl: Hatari ya mamlaka na nguvu za rais Donald Trump

Ines Pohl | Caro Robi
15 Mei 2018

Cheche za moto na mapigano katika Ukanda wa Gaza baada ya kufunguliwa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem ni uthibitisho tosha kuhusu hatari ya mamlaka na nguvu za Rais Donald Trump anasema mhariri mkuuu wa DW Ines Pohl.

https://p.dw.com/p/2xkFW
Ines Pohl Kommentarbild App
Picha: DW/P. Böll

Ni kipi kitamsukuma Donald Trump kusherehekea ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem wakati wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuondolewa kwa Wapalestina kutoka taifa jipya la Israel mwaka 1948? Uwanja wa ubalozi huo mpya wa Marekani unapindukia hadi Jerusalem Mashariki, eneo ambalo Wapalestina wana azma ya kuwa mji wao mkuu iwapo siku moja pia nao watakuwa na taifa lao.

Kuwepo kwa ubalozi huo ni pigo la kidiplomasia kwa Wapalestina wengi. Na licha ya kuwa hilo halihalalishi kuzuka kwa ghasia, hata hivyo ni uchokozi wa kimakusudi kutoka kwa Marekani.

Hiyo inamaanisha kuwa Rais wa Marekani anabeba dhamana ya mauaji ya Wapalestina wengi waliouawa Jumatatu ya tarehe 14 Mei pamoja na mamia ya waliojeruhiwa katika maandamano ya kupinga kuhamishwa kwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.

Kuvuruga makubaliano ya Iran

Ni kipi kitamsukuma mtu huyu kuyavuruga makubaliano kuhusu mpango wa kinyukila wa Iran yaliyochukua juhudi nyingi kufikiwa?

Kwa kutia tu saini yake kiholela kujiondoa kutoka makubaliano hayo, na bila hata kuwa mstaarabu kushauriana na wenzake wa nchi za Ulaya ili kujadili njia muafaka ya kushughulikia makubaliano hayo, kwa kujichukulia maamuzi, Trump ameonesha utayari wake wa kuitumbukiza hata zaidi kanda ya Mashariki ya Kati katika msukosuko na kutupilia mbali mahusiano ya amani kati ya Marekani na nchi za Ulaya ambayo yamedumu kwa miaka 70.

USA Donald Trump Ausstieg aus Atomabkommen mit dem Iran
Rais Trump akitia saini amri kuiondoa Marekani makubaliano ya nyukilia ya IranPicha: picture-alliance/abaca/D. Olivier

Ni kipi hasa kinampa msukumo mtu huyu ambaye anaonekana kutumia kila hila na njia kuyafutulia mbali kila mafanikio ya mtangulizi wake bila ya kuwa na hata mpango wowote wa kipi kitafuata baada ya kuyavuruga mafanikio hayo?

Donald Trump hakuwahi kipindi cha nyuma kuwa mwanasiasa aliyechaguliwa. Hakutayarishwa vyema kujitosa katika ulingo huo wa siasa ambao ni wa nipe nikupe, kujitolea na kupima faida na hatari za maamuzi.

Wanasiasa hutafakari kwa undani athari za matendo yao ikiwemo itaathiri vipi mustakabali wa siku za usoni.

Unahitaji tu kutizama nembo aliyotumia kuwakilisha mamlaka yake. Herufi za rangi ya dhahabu za jina lake zilizowekwa kwenye jengo lake la Trump Tower zinatupa mukhtasari wa anavyojiona: Kuwa  mimi ndiye bora zaidi na na nina uwezo wa kufanya lolote.

Huenda aliingia madarakani kwa kunadi sera kuwa Marekani kwanza lakini ukweli ni kuwa ujumbe anaoutoa ni kuwa ni Donald Trump kwanza

Hakuna njia Mbadala

Haya si mpya lakini matukio ya hivi karibuni yanadhidhirisha mamlaka makubwa ambayo yanaweza kuangamiza aliyo nayo mtu huyu. Trump hana mpango mbadala. Anapochukua maamuzi hafikirii matokeo yake, hajali ni kwa kiasi gani matendo yake na maneno yake yanavyoziathiri nchi nyingine zaidi ya Marekani.

Verleihung Internationaler Karlspreis an Macron
Kansela Angela Merkel na rais Emmanuel Macron Picha: Reuters/W. Rattay

Anajitamba kwa mamlaka aliyo nayo kwasababu ana uwezo huo, akiwa na lengo la kujipatia umaarufu kwa kila namna na hilo ni rahisi kulifikia pale ambapo kwa njia ya kiholela, unapanda mbegu ya maangamizi.

Ndiyo maana kachagua siku ya kihistoria kwa Wapalestina kufungua ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem na ni sababu hizo hizo, kaamua kuponda ponda makubaliano ya kinyuklia kuhusu Iran bila ya kuwaza ni kipi kitafuata.

Zinduka Ulaya!

Kwa Ulaya na Ujerumani matukio haya yanapaswa kuwazindua. Miongo saba baada ya kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia ni wakati kwa Ulaya kukua. Na hiyo inamaanisha kuchukua dhamana kwa sera za kigeni na masuala ya kiusalama.

Ujerumani inapaswa hatimaye kuzinduka na kuanza kuwekeza katika majeshi yake tena hata kama Wajerumani wengi katika kipindi cha nyuma walipendelea jeshi ambalo halijawezeshwa ipasvyo kwa ajili ya shughuli za kujilinda.

Uingereza nayo inahitaji kujitokeza bayana na kuona ni kwa jinsi gani inanuia kushirikiana na Ufaransa na Ujeumani kuhusu masuala ya kiusalama na ulinzi na Umoja wa Ulaya unahitaji kutafuta njia za kukomesha mivutano yaliyomo kwenye umoja huo na kuibuka kama asasi yenye nguvu yenye maono ya wazi kuhusu ni jamii gani ingependa watu wake waishi.

Kuna changamoto kubwa lakini jambo moja ni bayana, mtu hapaswi na asiitegemee nchi ambayo inaongozwa na mtu kama Donald Trump. Hatuhitaji kutizama mbali kupata ushahidi wa hatari iliyopo, matukio yanayojiri katika ukanda wa Gaza ni udhihirisho tosha!

Mwandishi: Ines Pohl

Tafsiri: Caro Robi

Mhariri: Iddi Ssessanga