Iran na Uturuki zaiunga mkono Qatar
26 Juni 2017Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson amesema Qatar imeanza kupitia matakwa ya nchi jirani za Kiarabu ili kuweza kumaliza mgogoro wa kidiplomasia unaoendelea kati yao kwa wiki kadhaa, na amezitolea wito pande mbili za mataifa ya Ghuba yanayozozana kukaa kitako kwa mazungumzo.
"Qatar imeanza kupitia orodha ya matakwa yaliyowasilishwa na Bahrain, Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu," amesema Tillerson katika taarifa yake aliyoitoa mjini Washington. "Ingawa baadhi ya vipengele vitakuwa ni vigumu sana kufikiwa na Qatar, lakini kuna maeneo muhimu ambayo yanatoa msingi wa kuendeleza mazungumzo yatakayopelekea kupatikana suluhisho."
Uturuki yakataa madai ya nchi za Kiarabu
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekataa madai ya nchi hizo za Kiarabu kuitaka Uturuki kuondoa wanajeshi wake kutoka Qatar, yakiwa ni miongoni mwa masharti mengine kadhaa ambayo Marekani imeyataja kuwa ni "vigumu kutekelezeka."
Akizungumza baada ya houba ya sikukuu ya Eid al-Fitr katika sala ya asubuhi mjini Istanbul, Erdogan amesema madai hayo ya nchi za Kiarabu ya kuitaka Uturuki kuwaondoa wanajeshi wake yamekosa heshima na kuongeza kwamba nchi yake haihitaji ruhusa ya nchi nyingine wakati wa kufanya makubaliano yake ya ushirikiano wa ulinzi.
"Tunakubali na kufahamu mtazamo wa Qatar dhidi ya orodha ya masharti hayo 13. Tunatambua kwamba njia hii ya madai 13 ni kinyume na sheria za kimataifa kwa sababu huwezi kushambulia au kuingilia nchi huru kulingana na sheria za kimataifa," amesema Recep Tayyip Erdogan.
Iran pia yaiunga mkono Qatar
Rais wa Iran Hassan Rouhani pia amesema jana kwamba anaiunga mkono Qatar katika kukabiliana na hasimu wa Iran - Saudi Arabia - pamoja na washirika wake kadhaa, na kusema kwamba kitendo cha "kuizingira Qatar hakikubaliki."
Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Bahrain zilikata mahusiano na Qatar mnamo Juni 5, kwa madai kwamba nchi hiyo inasaidia makundi ya kigaidi yenye misimamo mikali ya kidini, madai ambayo Qatar imeyakana.
Mataifa hayo ya Kiarabu yamewasilisha matakwa 13 kwa Qatar ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa kituo cha habari cha televisheni cha Al-Jazeera, kukata uhusiano na Iran, kufunga kambi ya kijeshi ya Uturuki iliyopo nchini humo na kulipa fidia.
"Iran inasimama pamoja na taifa la Qatar na serikali yake... Tunaamini na kwamba ikiwa kuna mgogoro kati ya nchi za kikanda, shinikizo, vitisho, au vikwazo si njia sahihi ya kutatua tofauti zao," Shirika la habari la serikali la Iran IRNA limemnukuu Rouhani akimwambia mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani katika mazungumzo ya simu.
Qatar ambayo majirani zake wamesitisha safari zote za anga kuelekea nchini humo, imesema inapitia masharti hayo 13 lakini pia imeyataja kuwa ni madai yasiyokuwa na busara au hayatekelezeki.
Iran amabyo ina wingi wa Waislamu wa madhhebu ya Kishia na Saudi Arabia yenye wingi wa Waislam wa madhahebu ya Kissuni, zinashutumiana kwa kudunisha usalama wa kikanda na kuunga mkono pande tofauti katika migogoro ya Syria, Yemen na Iraq.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpae/ape
Mhariri:Josephat Charo