Iran yaikamata meli ya mafuta huku wasi wasi ukiongezeka
18 Julai 2019Meli hiyo ilikuwa imebena lita milioni moja za mafuta wakati ilipokamatwa wakati ikipita katika ujia wa maji wa Hormuz , kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, ambalo halikusema ni taifa gani meli hiyo inatoka ama inatoa huduma kwa kampuni gani. Eneo hilo la ghuba ni moja kati ya maeneo muhimu ya njia ya majini kwa ajili ya kusafirisha mafuta. Iran imesema meli iliyokamatwa ni ile ambayo ilivutwa na kuondolewa katika eneo la bahari siku ya Jumapili baada ya meli hiyo kutuma ujumbe wa kuwapo na matatizo.
Maafisa wa marekani walisema jana kuwa hawana hakika iwapo meli ya mafuta iliyokuwa ikiondolewa kwa kuvutwa na kuingia katika eneo la maji la Iran imekamatwa ama kuokolewa. Uingereza imeiomba Iran kutuliza hali ya wasi wasi katika eneo la ghuba, wakati wakiahidi kulinda maslahi ya meli zake katika eneo hilo.
Eneo hilo limekuwa eneo tete wakati hali ya wasi wasi ikiendelea kuongezeka kati ya Iran na Marekani kuhusiana na kuvunjika kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani na hofu inaongezeka kuwa pande hizo mbili zinasogea karibu na makabiliano ya kijeshi.
Shutuma za Marekani kwa Iran
Ujia wa maji au mlango bahari wa Hormuz hivi karibuni umekuwa eneo la matukio kadhaa yanayohusu meli za kibiashara.
Mapema mwezi huu Uingereza iliikamata meli ya mafuta ya Iran nje ya eneo mla Gibraltar. Siku kadhaa baadaye Uingereza iliishutumu Tehran kwa kujaribu kuzuwia njia ya meli moja ya mafuta ya Uingereza katika ujia huo wa maji.
Marekani imeishutumu Tehran wa kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya meli za kibiashara karibu na ujia huo wa maji.
Tangu rais Donald Trump kuingia madarakani mwaka 2017, Marekani imeelekeza nguvu zake katika kampeni ya kuiwekea mbinyo mkubwa Iran , ikiwa ni pamoja na kujitoa kutoka katika makubaliano ya kinyuklia na mataifa yenye nguvu duniani na Iran mwaka 2015.
Mwezi uliopita Trump alisema alifikia karibu na kuamuru mashambulizi ya anga kwa kulipiza kisasi dhidi ya Iran kuiangusha ndege ya Marekani ya ujasusi isiyokuwa na rubani karibu na ujia huo.
Wizara ya ulinzi hivi karibuni imesema itaweka vikosi zaidi na meli katika eneo hilo katika juhudi za kuimarisha uchunguzi wa shughuli za Iran.
Rais wa Urusi Vladmir Putin na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamejadili kuhusu makubaliano ya kinyuklia na Iran pamoja na mzozo wa mashariki mwa Ukraine , imesema ikulu ya Urusi Kremlin leo. Ufaransa inajaribu kupunguza wasi wasi baada ya marekani kujitoa kutoka makubaliano hayo ya kinyuklia mwaka jana.