Iran yakanusha faulo katika ajali ya ndege ya Raisi
25 Mei 2024Raisi aliekuwa na umri wa miaka 63 alifariki siku ya Jumapili baada ya helikopta yake kuanguka katika eneo la milima kaskazini-magharibi mwa Iran, wakati akirejea kutoka kwenye uzinduzi wa bwawa la umeme kwenye mpaka na Azerbaijan.
Ripoti hiyo ya jeshi, imesema wachunguzi hawajakuta matundu yoyote ya risasi au athari sawa na hizo kwenye mabaki ya ndege hiyo, na kubainisha kuwa ilishika moto baada ya kugonga eneo la mwinuko.
Soma pia: Iran yamzika Ebrahim Raisi katika eneo takatifu zaidi la Kishia
Imesema pia hawakubaini chochote cha kutia shaka wakati wa mawasiliano kati ya marubani wa ndege hiyo na kituo cha uratibu wa mawasiliano ya safari za ndege. Raisi alizikwa siku ya Alhamisi katika mji wake wa nyumbani wa Mashhad.
Miongoni mwa watu wengine waliouawa katika ajali hiyo ni waziri wa mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian, ambaye pia alizikwa Alhamisi katika mji wa Shahre Ray, kusini mwa mji mkuu Tehran.