1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakiri wanajeshi wake wastaafu kushikwa mateka Syria

8 Agosti 2012

Vifaru vya serikali vimepenya ndani ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi mjini Aleppo jambo ambalo limezusha wasiwasi wa makundi ya haki za binaadamu, huku Iran ikikiri wanajeshi wake wastaafu ni miongoni waliotekwa Syria.

https://p.dw.com/p/15lcg
Wairani waliokamatwa na waasi wa Syria.
Wairani waliokamatwa na waasi wa Syria.Picha: picture alliance / dpa
  • Operesheni ya kuitwaa Aleppo kutoka mikononi mwa waasi yaanza
  • Waasi wakimbia maeneo yao
  • Iran yakiri "Walinzi wa Mapinduzi" washikiliwa mateka Syria

Uwezekano wa vikosi vya waasi kushindwa nguvu sasa ni mkubwa, licha ya kwamba bado vinashikilia karibu nusu ya mji wa Aleppo. Kamanda mmoja wa waasi hao, Wassel Ayub, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba asubuhi ya leo vifaru vya jeshi la serikali vimeingia kwenye wilaya ya Salaheddin, na kwamba mapigano makali yamezuka.

Kusonga mbele huko kwa jeshi la serikali ni baada ya jeshi hilo kuendesha mashambulizi ya mfululizo dhidi ya sehemu ya kaskazini magharibi mwa Aleppo kabla ya alfajiri, ambapo watu 12 wameuawa. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria.

Miongoni mwa waliouawa ni mwanamke mmoja na watoto wake wawili, ambao waliangukiwa na bomu kwenye nyumba yao iliyo kwenye kiunga cha al-Mashatiyyah. Viunga vingine vilivyoshambuliwa ni Qatarji, Tariq al-Bab na Sha'ar.

Picha za satalaiti zaonyesha matumizi ya silaha nzito

Mashambulizi haya yanafanyika katika wakati ambapo shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeelezea wasiwasi wake juu ya wakaazi wa Aleppo, likionesha picha za satalaiti zinazothibitisha kuongezeka kwa matumizi ya silaha nzito kwenye eneo hilo.

Kaburi la pamoja kwenye viunga vya Damascus.
Kaburi la pamoja kwenye viunga vya Damascus.Picha: picture-alliance/dpa

Shirika hilo limevitolea onyo vikosi vya Rais Bashar al-Assad kwamba vitabebeshwa dhamana za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu kutokana na kile kinachoendelea sasa Aleppo na kwengineko nchini Syria.

"Amnesty International inatuma ujumbe wa wazi kwa pande zote mbili katika mapigano haya, kwamba mashambulizi yoyote dhidi ya raia yataripotiwa vyema na wahusika watabeba dhamana kwa mujibu wa sheria za kimataifa." Amesema msemaji wa shirika hilo, Christoph Koettl, katika taarifa yake.

Picha kutoka Anadan, mji mdogo karibu na Aleppo, zinaonesha kuwa mabomu 600 ya kurushwa kwa mizinga yalivurumishwa kwenye eneo hilo.

Iran yakiri wanajeshi wake wastaafu kukamatwa na waasi Syria

Katika hatua nyengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, amesema hivi leo kwamba wanajeshi wastaafu wa Kikosi cha Mapinduzi cha nchi yake ni miongoni mwa mateka 48 wanaoshikiliwa na waasi nchini Syria.

Mjumbe wa kiongozi wa kidini wa Iran, Saeed Jalili (kushoto) akizungumza na Rais Bashar Assad wa Syria.
Mjumbe wa kiongozi wa kidini wa Iran, Saeed Jalili (kushoto) akizungumza na Rais Bashar Assad wa Syria.Picha: picture-alliance/dpa

Akinukuliwa na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake nchini Uturuki, Salehi amesema wamo pia wanajeshi wengine wastaafu na baadhi yao kutoka wizara nyengine. Hii ni mara ya kwanza kwa Iran kukiri kwamba mateka hao wana uhusiano na jeshi.

Salehi aliwasili Uturuki jana kuzungumza na serikali ya nchi hiyo juu ya hatima ya mateka hao, ambao tangu kukamatwa kwake Iran imeshikilia kuwa ni mahujaji.

"Uturuki ina mawasiliano yake na upinzani nchini Syria. Kwa hivyo tunafikiria kuwa inaweza kuwa na jukumu kubwa katika kuachiliwa kwa mahujaji wetu." Alisema Salehi hapo jana wakati akiwasili nchini Uturuki.

Iran ni muungaji mkono mkubwa wa serikali ya Assad, na hapo jana mjumbe maalum wa kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, alikuwa na mazungumzo na Rais Assad, ambapo mjumbe huyo, Saeed Jalil, alirejelea msimamo wa Iran kwamba kamwe haitawacha Syria mkono.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/Reuters/AFP
Mhariri: Othman Miraji