Wairan wapiga kura kumchagua rais mpya
28 Juni 2024Wagombea wanne ambao wote ni watiifu kwa kiongozi wa juu zaidi nchini humo wanakabiliana vikali kwenye uchaguzi huu.
Kituo cha televisheni ya umma kilionyesha msururu wa watu waliojipanga kwenye vituo vya kupiga kura kwenye miji kadhaa nchini Iran ambako raia milioni 61 wanastahili kupiga kura hadi majira ya saa 12.00 za jioni ambako vituo vitafungwa rasmi, ingawa mara nyingi huwa vinachelewa kufungwa hadi majira ya usiku.
Soma pia: Ayatollah Ali Khamenei awaongoza Wairan kumuaga Raisi
Uchaguzi huu unafanyika katikati ya ongezeko la mivutano ya kikanda, inayotokana na vita kati ya Israel na Hamas, ambao ni washirika wa Iran huko Ukanda wa Gaza na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon, lakini pia ongezeko la shinikizo la Magharibi dhidi ya Iran kuhusiana na namna inavyoimarisha mipango yake ya nyuklia, tena kwa kasi kubwa.
Ingawa uchaguzi huo hautarajiwi kuleta mabadiliko makubwa kuelekea sera za Jamhuri hiyo ya Kiislamu, lakini matokeo yake huenda yakawa na athari katika mchakato wa kumpata mrithi wa kiongozi wa juu kabisa wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, mwenye miaka 85 na aliyekaa madarakani tangu 1989.
Baada ya kupiga kura yake hii leo Khamenei alizungumza na waandishi wa habari na kuendelea kuwatolea wito watu kujitokleza kwa wingi ili kuhakikisha wanachagua kiongozi atakayewaongoza kukabiliana na mgogoro unaochochewa na umma kutoridhishwa na hali ya kiuchumi na ukandamizwaji wa uhuru wa kisiasa na kijamii.
Soma pia: Ayatollah Ali Khamenei ataka Wairan wajitokeze kupiga kura
"Siku ya uchaguzi ni wakati wa furaha na msisimko mkubwa kwetu sisi Wairani, haswa wakati wa uchaguzi wa rais wakati kura ya watu itakapoamua rais wetu kwa miaka ijayo."
Idadi ya wapiga kura imekuwa ikipungua katika kipindi cha miaka minne, katika wakati ambapo idadi kubwa ya vijana ikionyesha kukerwa na kuchoshwa na misimamo mikali ya kijamii.
Kwa kuwa kura hizo zinahesabiwa kwa mikono, matokeo yanatarajiwa kuanza kutoka siku mbili zijazo kabla ya matokeo rasmi ya mwisho kutangazwa.
Soma pia: Mshirika wa Khamenei ajisajili kuwania urais Iran
Kama hakutakuwa na mgombea atakayeshinda kwa angalau asilimia 50 jumlisha moja, taifa hilo litalazimika kufanya duru ya pili kati ya wagombea wawili waliopata kura nyingi, Ijumaa ya kwanza baada ya matokeo ya kwanza kutangazwa.
Wagombea watatu wenye misimamo mikali na mmoja ambaye si maarufu sana na mwenye misimamo ya wastani anayeungwa mkono na kikundi cha wanamageuzi ambacho kwa kiasi kikubwa kimekuwa kikitengwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.
Soma pia: Marekani yasusia kutoa heshima kwa hayati Raisi
Wakosoaji wa utawala wa kidini nchini Iran wanasema kushuka kwa idadi ya wapiga kura kwenye uchaguzi wa miaka ya karibuni kunaonyesha kutokukubalika kwa mfumo huo.
Ni asilimia 48 tu ya wapiga kura walishiriki kwenye uchaguzi wa 2021 uliomwingiza madarakani Ebrahim Raisi. Na hata waliopiga kura kwenye uchaguzi wa bunge uliofanyika miezi mitatu walikuwa wachache kiasi ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha asilimia 41 tu.
Rais ajaye hatarajiwi kuja na sera yoyote nzito itakayoleta mabadiliko kwenye mpango wa nyuklia wa Iran ama kuhusu msaada kwa makundi ya wanamgambo kote kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati kwa kuwa masuala mazito ya kitaifa yako chini ya Khamenei mwenyewe ingawa rais anayeongoza serikali bado ana uwezo wa kushawishi utekelezwaji wa sera za nje na za ndani.