Iran yashutumiwa kimataifa kwa kumnyonga muandamanaji
9 Desemba 2022Mohsen Shekari, mwenye umri wa miaka 23, aliuawa kwa kunyongwa siku ya Alhamis kufuatia hukumu ya kifo dhidi yake. Alishtakiwa kwa madai ya kuziba barabara ya mjini Tehran na kumjeruhi afisa wa usalama mnamo Septemba 25. Makundi ya kutetea haki za binadamu yalilaani mashtaka dhidi yake na kuyataja kama kesi ya maonesho.
Mahakama ilisema Shekari alikamatwa baada ya kumshambulia kwa panga, afisa wa kikosi cha usalama kiitwacho Basii kilicho na mafungamano na kikosi cha juu zaidi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini humo.
Mnamo mwezi wa Novemba, mahakama ilimkuta na hatia iitwayo ‚Moharebeh", yaani uadui dhidi ya Mungu ambayo adhabu yake ni kifo katika jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Iran
Hukumu ya kifo dhidi yake ilichochea shutuma za kimataifa dhidi ya Iran na tahadhari nyingi kutoka kwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, kwamba kuna hatari ya hukumu zaidi za watu kunyongwa kutolewa.
Mashirika ya haki za binadamu yalaani kunyongwa kwa Shekari
Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limesema ‘‘lilihofishwa'' na hukumu ya kumuua shekari kwa kumtia kitanzi, kitendo kilicholaaniwa pakubwa pamoja na kesi dhidi yake waliyosema haikuwa ya haki.
"Kuuawa kwake kunadhihirisha hali ya ukosefu wa ubinadamu nchini Iran, chini ya mfumo wake wa sheria, ambapo washukiwa wengi wanakenuliwa meno na hali hiyo hiyo," limeongeza shirika la Amnesty International.
UN yaitaka Iran kusitisha kamatakamata ya waandamanaji
Mahmood Amiry-Moghaddam, ambaye ni mkurugenzi wa shirika la (IHR) linalofuatilia haki za binadamu nchini Iran lakini lenye makao yake mjini Oslo, amehimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kali kuizuia nchi hiyo ya Kiislamu kutotekeleza hukumu zaidi za vifo. "Mohsen Shekari alinyongwa baada ya kesi yake iliyoendeshwa kwa pupa, bila haki na bila kuwakilishwa na wakili," amesema.
Mwili wa Shekari ulizikwa saa 24 baada ya kuuawa na mazishi yake yalihudhuriwa na watu wachache wa familia yake, pamoja na maafisa wa usalama katika maziara ya Behesht-e-Zahra. Mtandao wa kijamii 1500tasvir uliripoti.
Kando na maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika katika miji mbalimbali ya Iran kufuatia kifo cha msichana wa miaka 22 Mahsa Amini, aliyekufa mwezi Septemba mikononi mwa polisi wa maadili kwa madai ya kutovaa Hijab, kunyongwa kwa Shekari kumechochea maandamano zaidi.
1,000 washitakiwa kwa kuandamana Iran
Waandamanaji katika wilaya za Chitgar mjini Tehran wamesikika wakipaza sauti wakisema "kifo kwa dikteta na kifo kwa Sepah" wakimrejelea kiongozi mkuu w akidini wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei pamoja na kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran.
Nchi za Magharibi zimeelezea ghadhabu zao.
Washington imetaja kunyongwa kwa Shekari kuwa kuongezeka kwa hali ya kusikitisha na imeapa kuiwajibisha serikali ya Iran kwa vurugu dhidi ya raia wake wenyewe.
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni ameelezea kukerwa kwake na "ukandamizaji huo usiokubalika” ambao alisema hautaondoa matakwa ya waandamanaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa ujerumani Annalena Baerbock pia alikuwa na ujumbe saw ana huo. "Kitisho cha kuwanyonga watu, hakitaua azma na nia ya uhuru,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter huku akikosoa kile alichokitaja kuwa kesi ya uongo.
Kufuatia tukio hilo, Ujerumani pia ilimuita balozi wa Iran aliyeko Berlin. Hayo ni kulingana na duru ya kidiplomasia lakini ambayo haikutoa maelezo zaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alielezea masikitiko na ghadhabu kufuatia tukio hilo na kuuhimiza ulimwengu kutopuuza "dhuluma ya wazi inayofanywa na utawala wa Iran kwa raia wake wenyewe.”
Ofisi ya mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa imesema imechukizwa na kunyongwa kwa Shekari.
Kulingana na shirika la Amnesty International, Iran huwanyonga watu wengi zaidi kila mwaka kuliko taifa lolote lile likiwemo China.
Shirika la IHR lasema vikosi vya usalama Iran vimewaua watu 458 katika ukandamizaji wao dhidi ya waandamanaji. Shirika hilo lilionya wiki hii kwamba tayari vikosi hivyo vimewaua zaidi ya watu 500 mwaka huu, hiyo ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka jana.
(AFPE)
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Mohammed Khelef