1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yazituhumu Uturuki, Jordan kuwasaidia waasi wa Syria

13 Julai 2012

Wakati serikali na waasi wakilaumiana kwa "mauaji ya maangamizi" katika jimbo la kati la Hama nchini Syria, Iran imezinyooshea kidole Uturuki na Jordan kuwasaidia wapiganaji wanaoipinga serikali ya Bashar al-Assad.

https://p.dw.com/p/15XNN
Mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali-Akbar Salehi.
Mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali-Akbar Salehi.Picha: picture-alliance/dpa

Shirika la Haki za Binaadamu la Syria linasema kwamba wanajeshi wa serikali wamewarushia risasi waandamanaji mjini Damascus na katika mji wa kaskazini wa Aleppo, na kwamba hadi sasa watu 29 wameuawa nchini kote.

Idadi hiyo inajumuisha wanajeshi 18 wa serikali, waasi saba na raia wanne. Mauaji haya ya leo yanafuatiwa na yale ya usiku wa kuamkia leo kwenye kijiji cha Tramseh, kwenye jimbo la kati la Hama, ambapo taarifa zinasema kuwa zaidi ya watu 150 wamepoteza maisha yao.

Huku kila upande ukimlaumu mwenzake kwa mauaji hayo ya maangamizi, na Umoja wa Mataifa umethibitisha kutokea kwa mapigano kwenye eneo hilo.

"Kutoka kwa watu wetu walioko kwenye jimbo la Hama, tunaweza kuthibitisha kuendelea kwa mapigano hapo jana, katika eneo la Treimsah, ambayo yalijumuisha vifaru, urushianaji wa risasi wa moja kwa moja na pia helikopta." Amesema mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Robert Mood.

Risasi kila pahala

Katika jimbo hilo la Hama, waandamanaji walibeba bendera za uhuru wa Syria huku wakisoma dua za kuwaombea waliouawa usiku wa jana kwenye kijiji cha Tramseh. Katika mji mkuu, Damascus, wanajeshi wa serikali wanaripotiwa kutumia risasi za moto kuwatawanya waandamanaji kwenye wilaya ya Nahr Aysha.

Mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan (kushoto), na mkuu wa ujumbe wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Jenerali Robert Mood.
Mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan (kushoto), na mkuu wa ujumbe wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Jenerali Robert Mood.Picha: picture-alliance/dpa

Mbali na Damascus na Hama, waandamanaji waliingia mitaani katika miji ya Aleppo, Hasrata na Rastan, wote wakipiga mayowe ya kutaka utawala wa Assad uangushwe.

Waandamanaji hao pia wamebeba mabango yanayomtaka mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan, aondolewe, wakimuita "kibaraka wa Assad na Iran".

Iran yazionya Uturuki, Jordan

Wakati hayo yakiendelea, mkuu wa majeshi wa Iran, Jenerali Hassan Firouzabadi, amezituhumu Uturuki na Jordan kwa kuwaruhusu waasi wa Syria kuishambulia nchi hiyo kupitia mipakani mwao.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad.
Rais wa Syria, Bashar al-Assad.Picha: Reuters

Akinukuliwa na shirika la habari la ISNA, Jenerali Firouzabadi amesema kwamba ni jukumu la majirani wa Kiislamu wa Syria kujizuia kuwaunga mkono magaidi na akazitaka nchi hizo kufunga mipaka yake.

Upinzani nchini Syria na mataifa ya Magharibi wanailaumu Iran kwa kuipa silaha serikali ya Syria, lakini naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran, Hossein Amir Abdolahian, amesema makundi ya kigaidi yanayoendesha mauaji nchini syria yanapata msaada kutoka mataifa ya jirani, na kwamba tayari nchi yake imeshamfahamisha hilo, mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria, Koffi Annan.

Tangu maandamano yaanze nchini Syria miezi 16 iliyopita, zaidi ya watu 17,000 wanaripotiwa kupoteza maisha yao, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman