1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq kuwafunga miaka 15 wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja

Sylvia Mwehozi
28 Aprili 2024

Bunge la Iraq limepitisha muswada unaopiga marufuku mahusiano ya watu wa jinsia moja na adhabu ya kifungo cha hadi miaka 15 jela.

https://p.dw.com/p/4fGjd
Bunge la Iraq huko Irbil
Bunge la Iraq huko IrbilPicha: Christophe Petit Tesson/dpa/picture-alliance

Bunge la Iraq limepitisha muswada unaopiga marufuku mahusiano ya watu wa jinsia moja na adhabu ya kifungo cha hadi miaka 15 jela. Hatua hiyo imelaaniwa na mashirika ya haki za binadamu yanayosema ni mashambulizi dhidi ya haki za binadamu.

Chini ya muswada huo uliofanyia marekabisho sheria ya kupinga biashara ya kujiuza ya mwaka 1988, watu waliobadili jinsia watafungwa miaka mitatu jela. Muswada uliopita, ulikuwa umependekeza adhabu ya kifo kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Soma: Wanaharakati Uganda wakosoa EU kutochukua hatua dhidi ya sheria ya LGBTQ

Muswada huo unataja kuwa mabadiliko ya jinsia ya kibaiolojia kulingana na tamaa za watu binafsi ni uhalifu na kuwaadhibu watu waliobadili jinsia na madaktari ambao hufanya upasuaji.

Mapenzi ya jinsia ni mwiko katika jamii ya kihafidhina ya Iraq, lakini hapakuwa na sheria ambayo ilitoa adhabu ya wazi dhidi ya watu wanaoshiriki vitendo hivyo.