Iraq yatangaza vita kuifurusha IS Mosul
17 Oktoba 2016Vikosi vya usalama vya Iraq vikungwa mkono na majeshi ya Marekani vimefanya mashambulizi kaskazini ya mji wa Mosul, hiyo ikiwa ni hatua ya kuukomboa mji huo kutoka mikononi mwa kundi la Dola la Kiislamu - IS. Helikopta zimeonekana zikitoa miale ya mashambulizi, kando na milio ya miripuko kusikika.
Katika operesheni hiyo iliyoanza mapema leo, majeshi ya Iraq kwa ushirikiano na Marekani yamefaulu kuvikomboa vijiji kumi na viwili kusini mwa Mosul. Hayo yametangazwa na runinga ya taifa la Iraq ikinukuu taarifa kutoka idara ya mawasiliano ya jeshi.
Navyo vikosi vya Kikurdi, Peshmerga, vimevikomboa vijiji saba vinavyopakana na mashariki ya Mosul. Hii ni baada ya vikosi hivyo kushambulia maeneo matatu. Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa vikosi vya Peshmerga, Brigadia Halgurd Hikmat, aliyeongeza kuwa vikosi vyao vimeshachukuwa udhibiti wa barabara kuu katika eneo hilo.
Mapema leo waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alitangaza kuanza kwa operesheni iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Luteni Jenerali Stephen J. Townsend ni kamanda wa muungano w apamoja katika operesheni hiyo na anasema "Mapema leo vyombo vya usalama vya Iraq vimeanza mashambulizi kukomboa Mosul kutoka kwa ISIL ambalo pia linaitwa DAESH. Operesheni hii katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq huenda itachukua wiki kadhaa au zaidi. Iraq inaungwa mkono na muungano wa washirika kadhaa kupata silaha, ujasusi, ushauri na udhibiti wa mashambulizi ya angani. Lakini bayana ni kwamba maelfu ya wanajeshi watakaoukomboa Mosul, wote ni wa Iraq"
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema wanajeshi wake pia watashirikishwa kwenye operesheni hiyo. Televisheni ya taifa ilitangaza taarifa fupi mapema leo, ikitangaza mwanzo wa operesheni hiyo ya kijeshi inayotazamiwa kuwa ngumu na iwapo itafanikiwa litakuwa pigo kubwa zaidi kwa kundi hilo la itikadi kali.
"Leo natangaza kuanza kwa operesheni ya kishujaa kuwakomboa kutoka kwa Daesh. Mwenyezi Mungu akipenda tutakutana Mosul kusherehekea ukombozi na uokozi wenu kutoka kwa IS ili tuweze kuishi kwa pamoja tena, dini zote zikiungana na kwa pamoja tutaishinda Daesh ili tuujenge mji huu wa Mosul, alisema waziri mkuu Heidar al-Abadi kuptia televisheni ya taifa.
Waziri mkuu Al-Abad alijinasibu kuwafurusha kabisa wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kutoka nchini Iraq kabla ya kumalizika kwa mwaka huu. Al-Abadi alionyeshwa kwenye televisheni akiwa amevalia sare za kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi, huku akiwa amezungukwa na maafisa wandamizi wa jeshi.
"Vikosi hivi vinawakomboa leo, vina lengo moja tu mjini Mosul, ambalo ni kuwaondoa Daesh na kurejesha heshima yenu. Viko huko kwa ajili yanu," aliwambia wakaazi wa mji huo akituma jina mbadala la kundi hilo la wapiganaji. Mashuhuda walisema milio ya makombora ilianza kusikika katika ukanda wa Nineveh kuelekea Mosul. Televisheni ya taifa ilianza kupiga muziki wa kuhamasisha uzalendo dakika chache baada ya tangazo la waziri mkuu.
Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul itakuwa ndiyo kubwa zaidi nchini Iraq tangu majeshi ya Marekani yaondoke mwaka 2011 na ikiwa itafanikiwa, itakuwa ndiyo pigo kubwa zaidi kwa kundi hilo. Taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa Al-Abadi ilisema kuwa mapambano ya mji huo yanaashiria kuanza kwa awamu mpya itakayopelekea kukombolewa kwa ardhi yote ya Iraq kutoka kwa wapiganaji mwaka huu.
Marekani na washirika waahidi msaada
Mjini Washington, waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter aliutaja mwanzo wa operesheni hiyo kuwa ni wakati wa maamuzi katika kampeni ya kulisambaratisha kabisa kundi la Dola la Kiislamu. Carter alisema Marekani na mataifa mengine wanachama wa muungano wa kimataifa dhidi ya IS wako tayari kuvisaidia vikosi vya Iraq, wapiganaji wa Pershmerga na watu wa Iraq katika vita hii ngumu inayosubiri.
Vikosi vya Iraq vimekuwa vikijikusanya karibu na mji huo katika siku za karibuni. Vinahusisha wanajeshi wa kikosi maalumu ambao wanatarajiwa kuongoza harakati za kuingia mjini humo. Duru za kijeshi nchini Uturuki zimesema karibu wanajeshi 1,500 wa Iraq waliopewa mafunzo na Uturuki pia wanashiriki operesheni ya kuukomboa mji huo ambao ni nyumbani kwa raia zaidi ya milioni moja.
Mji wa Mosul uliangukia mikononi mwa IS wakati wa mashambulizi makali Juni 2014 na kuitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wake mbaya zaidi tangu uvamizi wa Marekani mwaka 2003. Baada ya kuiteka Mosul, kiongozi wa IS Abubakar al-Baghdadi aliutembelea mji huo na kutangaza himaya ya Kiislamu maarufu kama khilafa, ambayo kwa wakati mmoja ilichukua theluthi moja ya Iraq na Syria.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/John Juma/ape,dpae.
Mhariri: Daniel Gakuba