1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBurkina Faso

IRC: Mamilioni wakabiliwa na uhaba wa chakula Sahel

7 Mei 2024

Kamati ya kimataifa ya uokozi ya Marekani (IRC) imesema idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika mataifa yanayotawaliwa kijeshi katika ukanda wa Sahel imeongezeka.

https://p.dw.com/p/4fa4V
Chad Sahel | Njaa
Mwanamke akitembea kwa miguu, baada ya kuacha punda wake chini ya kivuli cha mti, ili mtoto wake achunguzwe kwa dalili za utapiamlo katika kituo afya cha Dibinindji, kijiji cha jangwani katika ukanda wa Sahel nchini Chad.Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa yake kamati hiyo imesema kiwango cha ukosefu wa chakula na utapiamlo kimeongezeka katika mataifa matatu ya Burkina Faso, Mali na Niger katika ukanda wa Sahel. IRC imesema watu milioni 7.5 wameathirika, kulinganisha na watu milioni 5.4 walioathirika mwaka jana.

Aidha IRC imetahadharisha kuwa hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi, na kuenea hadi katika nchi za Cameroon, Chad na Nigeria iwapo hakutakuwa na mavuno ya kutosha mnamo Juni hadi Agosti.

Soma pia: IRC yatahadharisha kuongezeka machafuko mkoa wa Darfur

Kulingana na makamu wa rais wa IRC Modou Diaw katika eneo la Afrika Magharibi na Kati, hali ya uhaba wa chakula imezidi kuwa mbaya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Diaw ameongeza kuwa mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa yanazidisha uhaba wa chakula, utapiamlo na ukosefu wa usalama, hali inayowasukuma watu kuyahama makaazi yao ndani na nje ya kanda.

Burkina Faso, Mali na Niger, ambazo ziliwekewa vikwazo vya kiuchumi vya kikanda baada ya mapinduzi ya Julai mwaka jana, zote zimo kwenye orodha ya Umoja wa Mataifa ya mataifa yenye maendeleo duni zaidi duniani.

Soma pia: Mabadiliko ya tabianchi yasababisha joto kali Sahel

Ripoti ya IRC imekwenda mbali zaidi katika kuchunguza jinsi maamuzi ya kisiasa kuanzia utawala wa kikoloni wa Ufaransa hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kutaja kamba maeneo ya pembezoni ya Sahel ya Kati yalitengwa kiuchumi na kisiasa.

Matokeo yake idadi kubwa ya watu katika Sahel ya kati wanakabiliwa na umaskini uliokithiri.

Kujitenga na koloni za zamani

Saint Petersburg- Rais Putin na Burkina Faso Traore
Rais wa Mpito wa Burkina Faso Ibrahim Traore (Kulia) na Rais wa Urusi Vladmir Putin wakipeana mikono wakati wa mkutano.Picha: Alexander Ryumin/dpa/Tass/picture alliance

Mataifa hayo matatu yamewafukuza wanajeshi wa Ufaransa, mtawala wake wa zamani, na mnamo Septemba walianzisha makubaliano ya ulinzi wa pande zote, ujulikanao kama Muungano wa Mataifa ya Sahel, na kugeukia zaidi Urusi kwa msaada.

Siku ya Jumamosi, washauri zaidi wa kijeshi wa Urusi walifika nchini Niger, wakileta vifaa vya kijeshi lakini pia chakula na bidhaa za kimsingi.

Takriban watu milioni 70 wanaishi katika mataifa hayo matatu, ambayo yote yanapambana na ghasia za wanamgambo wenye itikadi kali.