IS huenda ikatumia silaha za sumu Mosul
19 Oktoba 2016Majeshi ya Marekani yameanza kuokota mabaki ya makombora na kuyafanyia uchunguzi iwapo yalitengezwa na sumu ikizingatiwa wanamgambo wa IS walianza kutumia silaha hizo miezi michache kabla ya kuanza operesheni ya Jumatatu ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa IS.
Maafisa wa kijeshi wa Marekani wanaamini wanamgambo hao huenda wakajaribu kutumia silaha hizo kuwadhuru wanajeshi wa serikali ya Iraq na wapiganaji wa kikurdi na wa kishia wanaoshiriki katika operesheni hiyo kubwa dhidi yao.
Kuna takriban wanajeshi 5,000 wa Marekani nchini Iraq na mia kati yao wanashiriki katika operesheni hiyo ya kuukomboa mji wa Mosul kwa kusaidia katika kutoa ushauri wa kijeshi na mashambulizi ya angani dhidi ya ngome za kundi la Dola la Kiislamu.
Inakadiriwa kuna raia milioni moja mjini humo na Umoja wa Mataifa umeonya operesheni hiyo ya kijeshi huenda ikasababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu. Kuwepo kwa idadi kubwa ya raia ni changamoto kwa majeshi yanayojaribu kuwatokomeza wanamgambo wa IS.
Mkuu wa shirika la kimataifa kuhusu uhamiaji IOM nchini Iraq Thomas Weiss amesema inahofiwa wanamgambo wanawatumia raia kama ngao na kuongeza anatiwa wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutumiwa kwa silaha za sumu wakati ambapo hawajaweza kupata barakoa za kutosha kuwalinda raia.
Maelfu ya raia wameutoroka mji huo na kuelekea miji inayodhaniwa kuwa salama nchini humo huku wengine wakikimbilia nchi jirani ya Syria ambayo nayo inakumbwa na vita na kitisho cha IS.
Inaripotiwa kuwa kiongozi wa IS ni miongoni mwa wanajihadi sugu ambao wamesalia Mosul, mji wa pili kwa ukubwa Iraq na hivyo kuashiria kuwa mapambano yatakuwa makali. Maafisa wa Marekani wanaamini kuwa baadhi ya wapiganaji stadi wa IS wako mjini humo. Kuna kati ya wapiganaji 3,000 hadi 4,500 wa IS mjini Mosul.
Hii leo majeshi ya Iraq na washirika wake yanajiandaa kuukomboa mji wa Qaraqosh ambao wengi wa wakaazi wake ni wakristo. Majeshi yamewasili katika mji huo ulioko kilomita 15 kusini mashariki mwa Mosul.
Taarifa za mipango ya kuukomboa mji huo kutoka kwa IS zimesababisha sherehe miongoni mwa wakristo waliokuwa wameukimbia mji huo na kukimbilia Arbil. Qaraqosh ndiyo mji mkubwa zaidi miongoni mwa miji na vijiji vya Wakrtisto iliyodhibitiwa na IS katika eneo la Nineveh tangu mwezi Agosti mwaka 2014.
Hatua muhimu zimepigwa na maelfu ya wanajeshi wanaousogelea mji wa Mosul kutoka kila pande tangu siku ya Jumatatu lakini viongozi wa dunia na makamanda wa kijeshi wameonya kuwa licha ya hatua za mapema kupigwa, kuukomboa mji wa Mosul, huenda ikawa kazi ngumu mno na itakayodumu kwa wiki, miezi na hata miaka kadhaa ijayo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi kuhusu mapambano hayo na kuwatakia majeshi ya Iraq na washirika wake kila la kheri katika azma yao ya kuukomboa mji huo muhimu ambao ni ngome ya wanamgambo hao.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp
Mhariri: Gakuba Daniel