1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS yaukaribia mji wa Kobani

Admin.WagnerD3 Oktoba 2014

Mapigano makali yameripotiwa leo kati ya wanamgambo wa kikurdi na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS katika mji uliozingirwa karibu na mpaka baina ya Uturuki na Syria.

https://p.dw.com/p/1DPOO
Wakurdi wa Syria wakitimka kukimbia mapigano Karibu na mji wa Kobane
Wakurdi wa Syria wakitimka kukimbia mapigano Karibu na mji wa KobanePicha: Getty Images/B. Kilic

Wapiganaji wa Dola la Kiislamu IS wamesonga mbele hadi umbali wa kilomita chache nje ya mji huo wa Kobani ambao unajulikana pia kama Ain al-Arab kwa lugha ya kiarabu, licha ya mashambulizi ya anga ya jeshi la Marekani kuwasaidia wanamgambo wa kikurdi.

Miungurumo ya silaha nzito imesikika katika maeneo ya mpakani baina ya Syria na Uturuki, ikiambatana na moshi mweupe uliofuka katika maeneo hayo, hii ikiwa kwa mujibu wa waandishi wa habari walioshuhudia.

Kulingana na taarifa kutoka shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao nchini Uingereza, miripuko na moshi vilivyoshuhudiwa vilitokana na vifaru viwili vya IS ambavyo vimepigwa vilipokuwa vikiukaribia mji wa Kobane.

Wakurdi walalamika

Makundi ya wakurdi yameishutumu Uturuki kwa kuyafumbia macho maovu yanayofanywa na IS, na kuwakataza wakurdi wa Uturuki kuvuka mpaka kuwasaidia wenzao ndani ya Syria.

Mkurdi raia wa Uturuki ambaye amekwenda kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Syria, Cafer Seven amesema na hapa namnukuu, ''Tunaangalia kwa hofu mauaji yanayofanywa na kundi la IS, tukiwa na huzuni kubwa kutokana na jinsi ndugu zetu wanavyoteswa na ukatili wa kundi hilo'', mwisho wa kumnukuu.

Bunge la Uturuki limepiga kura kuidhinisha nguvu za kijeshi dhidi ya IS
Bunge la Uturuki limepiga kura kuidhinisha nguvu za kijeshi dhidi ya ISPicha: Reuters

Wakati huo huo lakini bunge la Uturuki lilipitisha jana hatua za kijeshi dhidi ya kundi hilo la kijihadi, ambalo limeyateka maeneo makubwa ndani ya Syria na Irak na kuyaweka chini ya Dola la Kiislamu lililolitangaza.

Mchambuzi mmoja wa siasa za Uturuki, Profesa Serhat Guvenc amesema ridhaa ya bunge hilo inatoa ruhusa isiyo na mpaka kwa serikali kuhusu kundi la IS.

''Kulingana na tangazo lililochapishwa, ujumbe ninaoupata ni kwamba serikali inataka uwezo usio na kikomo, inataka uhuru kamili kuhusu maamuzi ya kutumia hatua za kijeshi kukidhi malengo mbali mbali, yawe ya kijeshi, kisiasa au kidiplomasia ambayo itayaona ni muhimu''. Amesema Guvenc.

Nguvu zaidi zahitajika dhidi ya IS

Taarifa zaidi kuhusu vita dhidi ya kundi hilo lijiitalo Dola ya Kiislamu ni kwamba Australia imetangaza kujiunga na muungano unaoongozwa na Marekani katika vita hivyo ndani ya Irak. Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema wizara yake imefanya mazungumzo na Ufaransa kuitaka nchi hiyo ishiriki pia katika operesheni dhidi ya IS ndani ya Syria.

Ushirika unaoongozwa na Marekani umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga dhidi ya IS tangu August
Ushirika unaoongozwa na Marekani umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga dhidi ya IS tangu AugustPicha: Getty Images

Nchi tano za kiarabu zinashirikiana na Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya IS ndani ya Syria, huku idadi kama hiyo ya nchi za Ulaya zikishiriki katika mashambulizi ndani ya Irak.

Marekani pia imepeleka wanajeshi wapatao 1,600 kulisaidia jeshi la Irak katika sekta ya mafunzo na taarifa, huku Canada pia ikiwa imetuma maafisa kadhaa wa kijeshi kutoa ushauri kwa makamanda wa jeshi la Irak.

Haya yanajiri wakati jeshi la Irak likipata shinikizo kubwa kutoka kundi la IS katika mkoa wa Anbar unaokaliwa na wasuni wengi, huku pia wapiganaji wa kikurdi katika maeneo ya kaskazini wakipata mafanikio hafifu licha ya msaada wa mashambulizi ya anga yanayofanywa na ushirika unaoongozwa na Marekani dhidi ya IS.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri:Yusuf Saumu