1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sasa ni Seneta anayejivunia kwa kutetea wenye ualbino

25 Septemba 2017

Idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi inakadiriwa kuwa ni mtu mmoja katika kila watu 15,000 katika nchi zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara, Afrika.

https://p.dw.com/p/2kgBY
Kenia Parlament Austritt Römisches Statut
Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Isaac Mwaura ni miongoni mwa viongozi wachache wenye ulemavu  wa ngozi kuwahi kushika nafasi kubwa serikalini. Amechaguliwa juzi kuwa Seneta, nafasi ambayo ni ya kwanza katika orodha tangu alipopata umaarufu mwaka 2013 akiwa ni mkenya wa kwanza mwenye ulemavu wa ngozi, kuingia bungeni.

Lakini kabla ya kupata mafanikio haya, Mwaura amepitia mengi ambayo yalikuwa ni  changamoto kwake.

Anasema akiwa mtoto alijiona ni wa kawaida kama watoto wengine nchini humo, hakuwahi kujitazama kwenye kioo, na kuiona ngozi yake ikiwa tofauti na yenye weupe usio wa kawaida.

 Lakini imani hiyo ya kujiona kuwa ni wa kawaida, ilipotea siku moja akiwa na miaka 12, siku hiyo alikuwa na marafiki zake akitoka shule. Pamoja na yeye alikuwepo mwenzake mwenye ualbino. Anasema alishangaa kuona mtu akiwanyooshea kidole na kuwaita albino.

Baada ya kuchekwa na wenzake, Mwaura alimsubiri mama yake arudi nyumbani.

Mwaura alilimbia shirika la habari la Reuters kuwa ``Nilimuuliza mama,  albino ni mtu gani, na kwa nini anaitwa albino wakati wote tuna majina yetu?``

Anasema baada ya mama yake kumueleza,  ghafla aliiona dunia  ni tofauti na sehemu ya hatari kuishi.

Ualbino unaonekana kama laana nchini Kenya, na watu wenye hali hiyo huitwa zeruzeru neno lenye maana  ya mzimu.

 Watu wenye ulemavu huo aghalabu huchekwa na kushambuliwa na mara kadhaa kuuawa. Katika nchi nyingi za Afrika, viungo vya miili yao vinaaminika kuleta utajiri na huthaminiwa zaidi katika imani za kishirikina.

 Mara kadhaa, wenye ualbino hutelekezwa na wazazi wao na hawapelekwi shule kwa sababu wanaonekana wamedumaa kiakili.

Mwaura anbaye ambaye anaongoza kipindi cha redio kila jumamosi anatarajiwa kuibadilisha hiyo imani potofu.

 Aliwahi kuandaa mashindano ya urembo kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi mwaka 2016 ili kuondoa imani potofu.

Wataalamu wanasema kukataliwa kunaanza mapema. Watu wengi wenye ualbino nchini Kenya hulelewa na mzazi mmoja baada ya kukataliwa na wazazi.

Mwaura anasema  baba yake aliondoka nyumbani mara tu baada ya yeye kuzaliwa.  ``alisema siwezi kuwa mtoto wake``anasema Mwaura

Pamoja na changamoto zote hizo lakini Mwaura alifanikiwa kupata shahada ya kwanza na hatimaye ya pili nchini Afrika Kusini na Uingereza. Pia amefanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kuwa  mshauri wa kisiasa wa makamu wa Rais, mwaka 2010.

Changamoto hazikwisha, kwani hata alipokuwa bungeni, bado alidhihakiwa , kwa mfano kuna siku alivaa kofia kubwa ya  kuzuia jua na akaingia nayo bungeni. Mbunge mmoja alisimama na kuuliza kwa nini Cowboy ameingia ndani ya bunge.

Miongoni mwa mambo aliyoyafanikisha ni kuwashawishi wabunge kutenga fungu kwa ajili ya kulipia matibabu ya macho, saratani na vifaa vya kuzuia jua kwa watu wenye ualbino.

 Mwaka huu, Mwaura amefanikiwa kuwa Mkenya wa kwanza mwenye ulemavu wa ngozi kuingia bungeni kwa kupitia vyama vya mashinani akifahamika kama muthungu wa ruiru au mtu mweupe kutoka Ruiru eneo lililo kilometa 30  kutoka  jijini Nairobi.

Nchi jirani ya Tanzania, iliwahi kuwa na mbunge mwenye ualbino, mwaka 2010 na baadaye Abdallah Posi alichaguliwa kuwa Naibu Waziri na sasa ni balozi. Hali kadhalika nchi za Mali na Congo, kila moja ina waziri mwenye ulemavu huo.

Tansania Albino Salum Khalfan Barwany
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

 

 Mwandishi: Florence Majani

Mhariri: Saumu Yusufu