1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Hamas zaelekea kwenye mgogoro mkubwa Gaza

Admin.WagnerD8 Julai 2014

Ndege za kivita za Israel zilifanya mashambulizi makubwa katika ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia Jumanne, baada ya wapiganaji wa kundi la Hamas kufyatua maroketi kadhaa ndani ya kusini mwa Israel.

https://p.dw.com/p/1CY1D
Israel Westjordanland Konflikt
Picha: SAID KHATIB/AFP/Getty Images

Msemaji wa jeshi la Israel Peter Lerner alisema jeshi la angani la nchi hiyo liliyashambulia maeneo karibu 50 kwa mabomu usiku kucha, na kuonya kuwa Israel itaongeza taratibu ukubwa na ubora wa mashambulizi yake.

Haya ndiyo yalikuwa mashambulizi makubwa zaidi ndani na nje ya eneo hilo tangu November 2012, na yamekuja wakati Israel ikipambana kudhibiti wimbi la ghasia katika miji inayokaliwa na Waarabu kufuatia mauaji ya kinyama ya kijana wa Kipalestina yaliyofanywa na Wayahudi wenye itikadi kali.

Wapalestina wakiangalia uharibifu uliyofanywa kwenye makaazi yao mjini Gaza.
Wapalestina wakiangalia uharibifu uliyofanywa kwenye makaazi yao mjini Gaza.Picha: Reuters

"Operesheni ya kinga"

Mjini Gaza, wahudumu wa afya walisema watoto saba na wanawake wawili ni miongoni mwa watu 17 waliojeruhiwa, na kwamba wawili kati ya hao walikuwa katika hali mbaya. Jeshi la Israel lilithibitisha kuwa limeanzisha kampeni ya angani liliyoiita "operesheni ya Kinga" inayonuwia kupunguza mashambulizi ya roketi kusini mwa Israel.

Msemaji wa jeshi Lerner amesema karibu maeneo 50 yalilengwa katika mashambulizi ya usiku kucha, zikiwemo nyumba za wapiganaji, vituo vya kufyetulia roketi na miundombinu mingine ya wapiganaji hao.

Duru za usalama kutoka ndani ya Palestina zimesema maeneo yaliolengwa ni zaidi ya 70. Walioshuhudia walisema nyumba kadhaa zilishambuliwa, hasa katika mji wa kusini wa Khan Yunis. Salim Slimi ni mmoja wa watu walioharibiwa nyumba zao.

"Majira ya 9:20 tulipata simu kutoka kwa jeshi wakituomba tuondoke katika nyumba yetu. Familia nzima iliondoka na tuliwaambia majirani na sote tuliziacha nyumba zetu. Dakika kumi baada ya sisi kuondoka wakaishambulia nyumba. Yote imeharibiwa," alisema Salimi Slimi, mkaazi wa mji wa Khan Yunis.

Hamas yatishia kupanua mashambulizi

Hamas imeonye kuwa mashambulizi ya Israel yamevuka kile ilichokiita msitari mwekundu, na tawi lake la kijeshi la Ezzedine al-Qassam Brigades, limesema katika taarifa kuwa ikiwa sera hii ya Israel haitakoma, watajibu kwa kupanua eneo la mashambulizi yao kwa kiwango kitakachowashangaza.

Jeshi lilisema maroketi 81 yalirushwa kusini mwa Israel jana Jumatatu, na karibu theluthi moja yalifyetuliwa katika kipindi kifupi cha jioni. Mapema leo, makombora mengine sita yalifyetuliwa. Mkuu wa timu ya huduma za dharura katika eneo linalopakana na ukanda wa Gaza Illan, alisema hawakuweza kulala usiku wa kuamkia leo.

Afisa wa Polisi wa Israel akionyesha mabaki ya roketi lililofyatuliwa kusini mwa Israel.
Afisa wa Polisi wa Israel akionyesha mabaki ya roketi lililofyatuliwa kusini mwa Israel.Picha: Reuters

"Leo tulikuwa na usiku wa kelele kwa upande wetu, kwa sababu Wapalestina walifyatua maroketi mengi upande wa Israel na tulipata matatizo mengi na raia waliojawa na hofu. Wameyakimbia makaazi yao tunakoishi."

Katika mkutano ulifanyika jana Jumatatu, baraza la usalama la Israel lililipa mamlaka jeshi kuongeza mashmabulizi yenye lengo la kuongeza shinikizo kwa Hamas. Waziri wa Fedha Yair Lapid, alisema mashambulizi hayo yanalenga kurejesha utulivu kusini mwa Israel.

Msemaji wa jeshi amethibitisha leo kuwa wanajeshi zaidi wamepelekwa karibu na Gaza ili kujitayarisha kwa mashambulizi ya ardhini, ikiwa kutakuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman