Israel na Wahouthi washambuliana kwa makombora
27 Desemba 2024Hii ni baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kuupiga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa unaodhibitiwa na waasi na maeneo mengine nchini Yemen. Mashambulizi ya Israel jana Alhamisi yalitokea wakati mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani – WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema yeye na timu yake walikuwa wakijiandaa kuondoka katika mji huo mkuu unaodhibitiwa na Wahouthi wa Yemen. Saa chache baadae Ijumaa, Wahouthi wamesema wamefyatuwa kombora kuelekea uwanja wa ndege wa Ben Gurion na kurusha droni kadhaa kuelekea mji wa Tel Aviv pamoja na meli moja katika Bahari ya Arabia.
Soma pia: Israel yashambulia miundombinu ya Wahouthi Yemen
Jeshi la Israel limesema mapema Ijumaa kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga ilidungua kombora lililofyatuliwa kutokea Yemen kabla ya kufika katika ardhi ya Israel.
Mamlaka ya safari za anga nchini Yemen imesema uwanja wa Sanaa ulipangwa kufunguliwa Ijumaa baada ya mashambulizi ambayo ilisema yalitokea wakati ndege ya Umoja wa Mataifa ilikuwa inajiandaa kuruka.
Jeshi la Israel halijaeleza kama lilifahamu wakati huo kuwa Ghebreyesus alikuwa Sanaa. Shambulizi la Israel lilijiri siku moja baada ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kudai kurusha kombora moja na droni mbili kuelekea Israel. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikemea kuongezeka kwa uhasama kati ya Israel na Wahouthi na akasema mashambulizi kwenye uwanja wa ndege wa Sanaa yanatia wasiwasi mkubwa. Huyu hapa msemaji wake, Stephanie Tremblay. "Wajumbe walikuwa wamemaliza majadiliano juu ya hali ya kibinadamu nchini Yemen na juu ya kuachiliwa kwa wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa na wengine walioko kizuizini. Mashambulizi ya anga ya leo yanafuatia mwaka mmoja wa vitendo vya Wahouthi na Bahari ya Shamu na kanda ambavyo vinatishia raia, utulivu wa kikanda na uhuru safari za majini."
Soma pia: Waasi wa Kihouthi Yemen waziteka afisi za Umoja wa Mataifa
Televisheni ya Wahuthi ya Al-Masirah imesema mashambulizi ya Israel yaliuwa watu sita. Mashambulizi hayo yaliyoilenga uwanja wa ndege, vituo vya kijeshi na vituo vya umeme katika maeneo ya waasi yalikuwa ni mara ya pili tangu Desemba 19 ambapo Israel imeyapiga maeneo nchini Yemen baada ya kombora la waasi kufyatuliwa kuelekea Israel.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametuma onyo kwa waasi hao, akisema Israel itaendelea na mashambulizi hadi itakapofanikisha malengo yake. Kauli hiyo iliungwa mkono na waziri wake wa ulinzi Israel Katz. "Kama tulivyosema - atakayeishambulia Israel, tutampiga. Tutawawinda viongozi wote wa Houthi, tutawapiga kama tulivyofanya katika maeneo mengine. Hakuna atakayeweza kukwepa k´mkono mrefu wa Israel. Tutawapiga ili kuondoa vitisho kwa taifa la Israel."
Wizara ya mambo ya nje ya Iran ililaani mashambulizi hayo ya Israel ikisema ni ukiukaji wa wazi wa amani ya kimataifa na usalama na uhalifu usiopingika dhidi ya watu wa Yemen.
Kundi la Hamas, ambalo viongozi wake wakuu wameuawa na Israel wakati wa vita katika Ukanda wa Gaza, wamelaani shambulizi hilo wakisema ni uchokozi dhidi ya ndugu zao wa Yemen.
Wahouthi wa Yemen wameongeza mashambulizi yao dhidi ya Israel tangu mwishoni mwa Novemba wakati usitishaji mapigano ulianza kutekelezwa kati ya Israel na kundi jingine linaloungwa mkono na Iran, la Hezbollah nchini Lebanon.
afp, ap, dpa, reuters