1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel, wanamgambo wa Kipalestina warushiana makombora Gaza

10 Mei 2023

Jeshi la Israel na wapiganaji wa Gaza leo wamerushiana makombora katika mapigano mabaya kabisa kushuhudiwa katika eneo la pwani la Palestina katika muda wa miezi kadhaa.

https://p.dw.com/p/4RABv
Israelische Palästinenser Angriff
Picha: Hatem Moussa/AP Photo/picture alliance

Moshi ulitanda kutoka katika eneo lenye wakaazi wengi, baada ya Israel kutangaza kuwa inayalenga maeneo ya kurushia makombora ya kundi la wapiganaji wa Islamic Jihad.

Watu 15 wameuawa

Wizara ya afya ya Gaza imesema watu wanne wameuawa, siku moja baada ya mashambulizi ya Israel katika maeneo ya Kipalestina kuwaua watu 15, wakiwemo wanamgambo watatu wakuu wa Islamic Jihad na raia 12 wakiwemo watoto wanne.

Mwandishi habari wa shirika la habari la Ufaransa, AFP huko Gaza, amesema ameshuhudia maroketi kadhaa yakirushwa na wapiganaji wa Kipalestina, huku afisa wa ngazi ya juu wa Israel akiwaambia waandishi habari kwamba zaidi ya maroketi 60 yalirushwa.

Israel Palästina Nahost-Konflikt
Wapalestina wakiandamana wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama vya IsraelPicha: JAAFAR ASHTIYEH/AFP/Getty Images

Mfumo wa kujilinda na makombora ya angani wa Israel, Iron Dome, umeyaharibu makombora yaliyorushwa katika anga ya mji wa pwani wa Ashkelon na kwenye maeneo mengine ya kusini.

Wanamgambo wa Palestina wamefyatua makombora hayo katika kujibu mashambulizi ya anga yanayoendelea ya Israel, baada ya jana Jumanne kuapa kuwa watalipiza kisasi. Jeshi la Israel limesema mashambulizi yake yaliwalenga wanamgambo waliokuwa wakielekea kwenye eneo la kufyatulia makombora kwenye mji wa Khan Yunis, kusini mwa Gaza.

Ujerumani yalaani ghasia Gaza

Wakati huo huo, Ujerumani imelaani vikali kuongezeka kwa ghasia huko Gaza. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Christofer Burger, amesema kuwa Israel kama ilivyo nchi nyingine, ina haki ya kujilinda yenyewe, kama ilivyoanishwa katika sheria ya kimataifa, lakini lazima izingatie kanuni za uwiano na kuwalinda raia muda wote.

Kwa mujibu wa Burger, Ujerumani imeshtushwa sana na mauaji ya raia kadhaa wasiohusika wakiwemo watoto.

Christofer Burger
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Christofer BurgerPicha: Janine Schmitz/photothek/'picture alliance

"Watu wa Gaza na Israel wana haki ya kuishi kwa amani na kuzingatia utu. Mnajua msimamo wetu wa kimsingi kuhusu hili. Tunaweza kulifikia vyema lengo ndani ya mfumo uliojadiliwa wa suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Mashariki ya Kati,'' alisisitiza Burger.

Kwa mujibu wa Burger, jambo muhimu zaidi ni kuzuia kuongezeka kwa mapigano na waathirika zaidi na kwamba Ujerumani inatazama ongezeko la ghasia Gaza kwa wasiwasi mkubwa. Amesema wale wote wenye dhamana wanapaswa kutekeleza jukumu lao kuzuia mapigano.

Katika hatua nyingine ambayo inaweza kuzidisha hali ya wasiwasi, polisi wa Israel wamesema kuwa wataruhusu gwaride la Wayahudi wenye kufuata siasa kali za kizalendo kufanyika wiki ijayo.

Gwaride hilo maalum kwa ajili ya kusherehekea kudhibitiwa kwa Jerusalem Mashariki na maeneo matakatifu ya Kiyahudi, hupita katikati ya makaazi ya Waislamu kwenye Mji Mkongwe na mara nyingi husababisha makabiliano na wakaazi wa Kipalestina.

 

(AFP, AP, Reuters)