1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaishambulia Beirut kabla ya usitishaji mapigano

26 Novemba 2024

Jeshi la Israel limeshambulia kwa mabomu mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na kuharibu jengo karibu na wilaya zenye idadi kubwa ya watu za Nuwairi na Ras al-Naba.

https://p.dw.com/p/4nRoT
Beirut-Lebanon
Beirut-LebanonPicha: AFP

Jeshi la Israel limeshambulia kwa mabomu mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na kuharibu jengo karibu na wilaya zenye idadi kubwa ya watu za Nuwairi na Ras al-Naba. Haya ni kulingana na walioshuhudia na vyanzo vya usalama.

Hata hivyo hakukuwa na ripoti za majeruhi au maelezo zaidi kuhusu tukio hilo. Jeshi la Israel halikutoa onyo kabla ya shambulizi.

Badala yake msemaji wa jeshi la Israeli alitoa onyo kwa karibu majengo 20 katika kitongoji cha mji mkuu wa Dahiyeh, ngome ya wanamgambo wanaoiunga mkono Iran Hezbollah. Kufikia mchana wa leo Israel imetahadharisha mara kadhaa kushambulia eneo la kusini mwa Beirut. Soma: Israel yatarajiwa kukubali mpango wa kusitisha mapigano na Hezbollah

Mkuu wa Shirika la Haki la Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake Jeremy Laurence, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa uhasama nchini Lebanon.

"Mashambulizi ya kijeshi ya Israel nchini Lebanon yamegharimu maisha ya raia wengi, ikiwa ni pamoja na mauaji ya familia nzima, ongezeko la watu kuachwa bila makao na uharibifu wa miundombinu ya kiraia, na kuibua wasiwasi mkubwa juu ya kuheshimiwa kwa kanuni za uwiano."

Haya yanajiri wakati Israel ikitarajiwa kufikia mpango wa kusitisha mapigani nchini Lebanon.