1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaitisha uchaguzi wa mapema Machi

Yusra Buwayhid
23 Desemba 2020

Israel imeitisha uchaguzi wa mapema utakaofanyika Machi 23, baada ya bunge kushindwa hapo Jumanne kuidhinisha bajeti ya serikali ikiwa ndiyo tarehe ya mwisho iliyopangwa kufanya hivyo.

https://p.dw.com/p/3n7w7
Israel Netanjahu
Picha: Yonatan Sindel/AP/picture alliance

Kushindwa kuidhinishwa bajeti kunaiporomosha serikali ya sasa ya muungano ya Israeli, iliyoundwa kati ya chama cha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na mpinzani wake mkuu, Benny Gantz, mnamo mwezi Mei, ili kupambana na changamoto za janga la virusi vya corona.

Lakini ushirikiano wao ulikumbwa na hali ya kutoaminiana na mivutano isiokwisha.

Mpinzani mkuu wa Netanyahu katika uchaguzi ujao ni Gideon Saar, mwanasiasa aliyejitenga kutoka katika chama cha waziri mkuu huyo cha Likud.

Soma zaidi: Benjamin Netanyahu apewa jukumu la kuunda serikali ya muungano

Utafiti wa maoni ya raia kabla ya uchaguzi unaonyesha kuwa Saar anamkaribia sana Netanyahu kwa umaarufu miongoni mwa wapigakura.

Hata hivyo baada ya bunge kuitisha uchaguzi mpya, Netanyahu alisema kuwa anaamini atashinda uchaguzi huo wa mwakani.

"Tunapinga uchaguzi, huu ni uamuzi mbaya wa Chama cha Bluu na Nyeupe, lakini ikiwa uchaguzi utalazimishwa, naahidi kwamba tutashinda," amesema Netanyahu.

Licha ya utabiri wake huo, Netanyahu mara hii atakabiliwa na hali ngumu zaidi tofauti na chaguzi zilizopita, kwani hatakuwa na uungwaji mkono wa mshirika wake Rais Donald Trump wa Marekani.

Netanyahu atakabiliwa na changamoto za uchaguzi

Soma zaidi: Pompeo: Marekani itaendelea kuipa kipaumbele Israel

Rais mteule Joe Biden ataapishwa rasmi mnamo Januari 20. Biden anatarajiwa kurudisha sera za rais wa zamani Barack Obama, ambaye hakuwa na uhusiano mzuri na Netanyahu kutokana na jinsi Israel inavyowakandamiza Wapalestina.

Israel Benjamin Netanjahu wird gegen COVID-19 geimpft
Benjamin Netanyahu akidungwa chanjo dhidi ya COVID-19Picha: Amir Cohen/REUTERS

Soma zaidi:Makundi ya Wapalestina yatangaza siku ya Ghadhabu

Aidha kampeni za uchaguzi wa nne wa bunge ndani ya miaka miwili, zitafanyika wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiwa anakabiliwa na changamoto kadhaa.

Miongoni mwao ni hasira ya umma inayotokana na jinsi alivyoshindwa kukabiliana na na janga la virusi vya corona, huku akiwa katikati ya kesi ya ufisadi, ya kwanza dhidi ya waziri mkuu wa Israel.

Kuhusiana na suala la janga la corona, wiki hii Netanyahu alifanikiwa kuifanya Israeli kuwa moja ya nchi za kwanza ulimwenguni kutoa chanjo kwa raia wake.

Lakini bado haijulikani ni watu wangapi wataweza kupewa chanjo hadi Machi. Huku Israeli ikikabiliwa na mlipuko mbaya wa virusi vya corona na hata uwezekano wa wananchi kuwekewa vizuizi kwa mara ya tatu. Wapiga kura wenye hasira wanaweza kumwadhibu Netanyahu kupitia visanduku vya kupigia kura kwa kuporomoka kwa uchumi hali iliyosababishwa na janga hilo.

Vyanzo: (rtre,ap)