1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiMashariki ya Kati

Israel yajibu tuhuma mbele ya ICJ

Angela Mdungu
12 Januari 2024

Timu ya wanasheria wa Israel imesema mbele ya mahakama ya Haki ya Kimataifa ICJ kuwa, nchi hiyo hailengi kuwaangamiza watu wa Palestina katika vita vyake kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4b9wB
Uholanzi | Mahakama ya Haki ya Kimataifa ICJ
Mahakama ya Haki ya Kimataifa ICJPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Hayo yameelezwa wakati Israel ikijibu tuhuma zilizotolewa na Afrika ya Kusini kuwa inafanya vitendo sawa na mauaji ya ya kimbari  katika operesheni yake ya kijeshi kwenye Ukanda huo.

Israel imeanza kujibu tuhuma hizo za Afrika ya Kusini ikiwa ni siku ya pili ya kuwasilisha hoja, mbele ya majaji wa Mahakama ya ICJ mjini The Hague. Israel katika mahakama hiyo imeitaka mahakama ya Kimataifa ya Haki kuyakataa matakwa ya Afrika ya Kusini yanayodai Israel ilaazimishe kusimamisha kampeni yake ya Kijeshi katika Ukanda wa Gaza.

Soma Afrika Kusini yaishutumu Israel kwa mauaji ya kimbari

 Alhamisi, ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, Afrika ya Kusini iliwasilisha hoja yake kuwa, Israel inafanya  vitendo vilivyopangwa kwa ustadi vya mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza, na imetoa mifano ya vitendo hivyo kuwa ni mashambulzii makali ya jeshi na kauli za wanasiasa wa Israel.

Uholanzi | Mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati
Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola na Balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi Vusimuzi Madonsela wakihudhuria Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kabla ya kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel iliyoletwa na Afrika Kusini, mjini The Hague Januari 11, 2024.Picha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP/Getty Images

Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza iliyo chini ya Hamas, hadi sasa zaidi ya Wapalestina 23,000 wameuwawa huku asilimia 70 ya idadi hiyo ikiwa ni wanawake na watoto kutokana na mashambulizi ya anga na ya ardhini yanayofanywa na jeshi la Israel katika Ukanda huo.

Mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake nchini Uholanzi inatarajiwa kutoa uamuzi wake baadaye mwezi huu kuhusu hatua za dharura zinazoweza kuchukuliwa.

Kesi kuhusu mauaji ya Kimbari itachukua muda kusikilizwa

Hata hivyo, kesi kuhusu tuhuma kuu za mauaji ya kimbari haitatolewa maamuzi katika wakati huo na huenda ikachukua miaka mingi kusikilizwa. Israel imetetea kutumia haki yake ya kujilinda baada ya mashambulizi ya kundi la Hamas na makundi mengine ya Wapalestina yenye itikadi kali yaliyofanywa Oktoba 7 mwaka uliopita.

Takriban watu 1,200 waliuwawa kutokana na shambulio hilo na wengine karibu 250 walitekwa nyara kutoka Israel ambapo nusu ya mateka hao wameshaachiliwa hadi sasa.

Uholanzi | Mahakama ya Haki ya Kimataifa ICJ
Mshauri wa masuala ya Kisheria wa Israel Tal Becker akiwa katika mahakama ya ICJPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Soma pia:Mahakama ya ICJ yaanza kusikiliza kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel 

Tangu vikosi vya Israel vilipoanzisha mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza, karibu watu wote milioni 2.3 wanaoishi Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao walau mara moja, hali ambayo imesababisha mgogoro wa kiutu.

Israel imeyapuuza madai ya Afrika ya Kusini ikisema kuwa hayana msingi wowote. Jana Alhamisi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu alisema kuwa mapambano dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza yanazingatia sheria ya kimataifa.

Afrika ya Kusini imekuwa ikiiunga mkono dhamira ya Palestina ya kuwa taifa, uhusiano ulioanza kati ya pande hizo wakati chama cha ANC kilipokuwa kikipambana dhidi ya utawala wa wazungu wachache nchini Afrika ya Kusini.