1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema imeshambulia ngome 12,000 za Hamas

2 Novemba 2023

Jeshi la Israel limesema limeshambulia zaidi ya ngome 12,000 za Hamas katika Ukanda wa Gaza tangu vita vyake dhidi ya kundi hilo kuanza.

https://p.dw.com/p/4YKYN
Majengo yaliyoharibiwa vibaya kufuatia mashambulizi ya Israel, Gaza
Majengo yaliyoharibiwa vibaya kufuatia mashambulizi ya Israel, Gaza Picha: STR/AFP

Israel imeyasema haya huku mapigano makali ya ardhini yakiendelea katika eneo hilo lililo ndani ya mamlaka ya Palestina. Wakati huo huo, mkuu wa jeshi wa Israel Luteni Jenerali Herzi Halevi amedokeza kuwa huenda Israel ikaondoa marufuku yake ya kupeleka mafuta katika Ukanda wa Gaza.

Akizungumza kwa njia ya televisheni Halevi amesema iwapo hospitali katika eneo hilo zitaishiwa huenda nishati hiyo ikaongezwa ila kwa usimamizi.

Israel ilifungia bidhaa muhimu ikiwemo nishati kuingia Gaza kufuatia shambulizi la Hamas la Oktoba 7.

Misri yawapokea majeruhi kutoka Ukanda wa Gaza

Huku hayo yakiarifiwa, mataifa ya Kiarabu ambayo yamerudisha mahusiano na Israel au yanakusudia kufanya hivyo, yanakabiliwa na shinikizo la umma linaloongezeka kusitisha mahusiano hayo, kutokana na vita vya Israel dhidi ya Hamas.

Makumi kwa maelfu ya watu wameingia mitaani leo katika Mji Mkuu wa Morocco Rabat na miji mingine wakiwaunga mkono Wapalestina.