Israel yasikitishwa na vifo vya wahudumu wa misaada Gaza
3 Aprili 2024Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi amesema leo katika ujumbe wa video kuwa shambulizi lililoupiga msafara wa shirika la hisani la World Central Kitchen – WCK uliokuwa unapeleka msaada Gaza Jumatatu wiki hii lilikuwa kosa kubwa. "Tukio hili lilikuwa ni kosa kubwa. Israel iko kwenye vita na Hamas, sio na watu wa Gaza. Tunasikitika kwa madhara ya kutokusudiwa kwa wahudumu wa WCK. Tunaomboleza pamoja na familia za waathiriwa na pia Shirika zima la Central Kitchen kutoka ndani kabisa ya mioyo yetu."
Hapo jana, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema jeshi liliwauwa bila kukusudia wafanyakazi wa misaada, na kusema ni tukio la kutisha, ambalo lingechunguzwa hadi mwisho. Hatahivyo, hakuomba msamaha.
Shambulizi, hilo liliwauwa Muastralia, Muingereza, Mpalestina, Mpoland, na mmoja mwenye uraia wa Marekani na Canada, lililaaniwa vikali, huku viongozi wa ulimwengu wakidai uchunguzi.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema tukio hilo na jinsi Netanyahu alivyolizungumzia vimesababisha hasira inayoeleweka na kuharibu mahusiano. Poland inataka famila za wahudumu hao waliouawa zilipwe fidia.
Kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa wito upya wa amani huko Gaza na Ukraine, akilaani mauaji ya wafanyakazi hao wa misaada.
Tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas Oktoba mwaka jana, shirika hilo la hisani la WCK lenye makao yake Marekani limekuwa likihusika katika kuwalisha wakazi wa Gaza waliopoteza makazi, na lilikuwa moja ya mashirika yanayoongoza uwasilishwaji wa msaada wa chakula unaowasili kupitia baharini kutokea Cyprus.
Katika taarifa iliyondikwa kwa maneno makali, Rais wa Marekani Joe Biden amesema Israel haijafanya vya kutosha kuwalinda wahudumu wa misaada wanaojaribu kupeleka msaada unaohitajika kwa dharura kuwasaidia raia.
Miili ya wafanyakazi sita wa kigeni imepelekwa leo kwenye mpaka wa kusini mwa Gaza kabla ya kusafirishwa katika nchi zao, kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa hospitali moja ya Rafah.
Vifo vya wafanyakazi hao wa msaada vinajiri wakati mashambulizi ya mfululizo ya Israel yakiendelea kuipiga Gaza, na kuharibu kabisa miundo mbinu muhimu, ikiwemo mfumo wa afya na kuwaweka zaidi ya nusu ya watu wa eneo hilo kwenye ukingo wa baa la njaa.
Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema leo mashambulizi ya Israel yamewauwa watu 66.
Mivutano ya kikanda pia imeongezeka baada ya Israel kulaumiwa kwa shambulizi la angani kwenye ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus Jumatatu ambalo liliwauwa maafisa saba wa Kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi, wawili wakiwa ni majenerali. Tehran, ambayo inaunga mkono Hamas na makundi mengine yanayopigana na Israel na washirika wake kote katika kanda hiyo, imeapa kulipiza kisasi.
afp, reuters, ap, dpa