Israel yashambulia uwanja wa ndege, bandari Yemen
27 Desemba 2024Israel ilifanya mashambulizi ya anga kwenye maeneo kadhaa yanayohusiana na Wahuthi nchini Yemen, yakiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa na bandari za Bahari ya Shamu, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua sita na kuwajeruhi kadhaa, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Wahuthi na Umoja wa Mataifa.
Mashambulizi hayo, ambayo pia yalilenga vituo vya umeme na miundombinu ya kijeshi, yalifuata mashambulizi ya makombora na droni ya Wahuthi dhidi ya Israel, yaliyotajwa kama ishara ya mshikamano na Wapalestina.
Soma pia: Netanyahu aahidi 'nguvu, dhamira' dhidi ya Wahuthi Yemen
Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alikuwa uwanjani wakati wa shambulio hilo, ambapo mfanyakazi mmoja wa ndege yake alijeruhiwa.
Kaskazini mwa Gaza, shambulio la anga la Israel liliua watu wasiopungua 50, wakiwemo wafanyakazi wa matibabu, huku askari mmoja wa Israel akiuawa katika mapambano yanayohusiana.
Umoja wa Mataifa umelaani mzozo huo, ukionya kuwa mashambulizi kwenye miundombinu ya Yemen yanahatarisha misaada ya kibinadamu, ambayo inategemewa na karibu asilimia 80 ya Wayemeni.
Wahuthi, ambao ni sehemu ya muungano wa Iran unaojulikana kama "mhimili wa upinzani," walitishia kujibu, hali inayochochea mvutano zaidi katika kanda hiyo.