1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashinikizwa kusitisha vita na Hamas

13 Februari 2024

Israel inashinikizwa kimataifa ikubali kusitisha vita vyake na kundi la Hamas, katika wakati taifa hilo linajitayarisha kufanya mashambulizi kwenye mji uliofurika watu wanaokimbia mapigano kusini mwa Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4cLft
Mkuu wa CIA William Burns
Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA William BurnsPicha: MANDEL NGAN/AFP/Getty Images

Mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, William Burns anakwenda mjini Cairo leo kwa duru nyingine ya mazungumzo akilenga kutanzua mkwamo wa kufikiwa makubaliano kwa rasimu ya mkataba mpya wa kusitisha vita uliotayarishwa na Qatar.

Safari yake inafanyika baada ya Marekani na Umoja wa Mataifa kuionya Israel dhidi ya kuushambulia mji wa Rafah bila kuwa na mpango madhubuti wa kuwalinda raia, ambao inaarifiwa hawana mahala pengine pa kwenda.

Hapo jana rais Joe Biden wa Marekani alikutana na Mfalme Abdullah II wa Jordan mjini wa Washington na kusisitiza kwa mara nyingine kuwa raia wanaokaribia milioni 1 kwenye mji wa Rafah "wanapaswa kulindwa".