Israel yasitisha hujuma kwa muda kuruhusu raia kuondoka
15 Desemba 2023Wakala wa serikali ya Israel unaoshughulikia masuala ya raia wa Palestina umesema katika mtandao wa kijamii wa X kuwa, usitishwaji huo wa muda unafanyika katika eneo la Al-Salaam huko Rafah kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane.
Tangazo hilo la Israel limetolewa katika wakati ambapo msimu wa mvua na baridi kali unazidisha masaibu ya wakaazi wa Gaza ambao tayari wameyakimbia makaazi yao.
Jana, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimueleza mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani, Jake Sullivan, kuwa Israel itaendeleza vita vyake dhidi ya Hamas hadi "ushindi kamili" utakapopatikana.
Wawili hao pia walijadiliana juu ya vitisho vya kikanda vikiwemo kutoka kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah na waasi wa Houthi wa Yemen, pamoja na juhudi za Israel kuwaokoa mateka.