Israel yazidisha mashambulizi Gaza
10 Julai 2014Vifo hivyo vimeongeza idadi ya watu waliouwawa kufikia 80 tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya angani siku ya Jumanne, dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Akizungumza na shirika la habari cha AFP msemaji wa huduma za dharura Ashraf al-Qudra amesema katika shambulizi la hivi karibuni mtoto wa miaka mitano aliuwawa wakati bomu kutoka Israel lilipofyetuliwa Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, katika mji wa Beit Lahiya.
Aidha mauaji mengi zaidi yalishuhudiwa katika mji wa Khan Yunis ambapo mkahawa mmoja ulishambuliwa wakati watu walipokuwa wakiangalia mechi ya kombe la dunia kati ya Argentina na Uholanzi, watu wanane waliuwawa huku wengine 15 wakijeruhiwa.
Saa moja baadaye ndege mbili za kivita za Israel zikashambulia nyumba mbili katika mji huo huo wa khan Yunis na kusababisha mauaji ya wanawake wanne na watoto wanne.
Ban Ki Moon alaani Mashambulizi ya Mashariki ya Kati
Hata hivyo mpaka sasa hapajakuwepo na mauaji yoyote ya raia wa Israel lakini Hamas imezindua mawimbi ya makombora, katika maeneo kadhaa nchini Israel.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anayetarajiwa kulihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa juu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, amelaani mashambulizi ya angani huku akiihimiza Israel kusimamisha mashambulizi.
"Kwa mara nyengine tena nalaani mashambulizi ya angani yanayofanywa na Israel katika ukanda wa Gaza, mashambulizi kama haya hayakubaliki na ni lazima yasimamishwe, pia namuomba Waziri Mkuu Netanyahu kusimamisha mashambulizi na kuheshimu majukumu ya kimataifa ya kulinda raia," alisema Ban Ki Moon.
Naye balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa awali alisema Baraza hilo la usalama la Umoja wa mataifa linajikokota kushughulikia mgogoro unaoendelea.
Huku hayo yakiarifiwa Misri imefungua mpaka wake wa Rafah ili kuwapokea raia wa palestina waliojeruhiwa. Hospitali Kusini mwa eneo la sinai linalopaka na Gaza pamoja na Israel zipo tayari kuwapokea raia hao waliojeruhiwa. Hii ni kulingana na shirika la habari la Misri MENA.
Mshindi wa tuzo la amani la Nobel Desmond Tutu pia ameongeza sauti yake katika mgogoro huu wa Mashariki ya kati na kusema viongozi wa Israel na Palestina wanabidi kuacha kulaumiana kama watoto katika mgogoro wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mhariri: Yusuf Saumu