Jeshi la Isreal lazivunja nyumba za Wapalestina
22 Julai 2019Wakiwa na trekta aina ya buldoza wanajeshi hao walibomoa majengo na nyumba zilizokuwa zinaishi watu katika kijiji cha Sur Baher kilichoko katika eneo hilo lililotekwa na kukaliwa na Israel katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967. Mwanaharakati wa Palestine katika mji jirani wa Wadi Al-Hummus alisema darzeni ya majengo yamezungushiwa vilipuzi yakitayarishwa kubomolewa huku wenyeji wakifurushwa.
Waziri Mkuu wa Palestine, Mohammad Shtayyeh amesema watapeleka malalamiko yao kwa mahakama ya kimataifa.
"Kikosi cha jeshi kimekuja asubuhi na kubomoa majengo karibia kumi na sita na nyumba katika eneo la Wadi Ummus katika kijiji cha Sur Bahe. Baraza la mawaziri linashutumu jambo hili baya sana. Huku ni kuendelea kuwafursuha kwa lazima wenyeji wa Jerusalam kutoka kwa majumba na ardhi zao - hivi ni vita vya kiuhalifu na uhalifu dhidi ya binadamu," alisema Shtayyeh.
Israel ilisema sababu ya kufanya hivyo ni kwa kwamba majengo hayo yamejengwa karibu sana na uzio walioujenga wa Ukingo wa Magharibi kwa hivyo ni hatari kwa usalama wao. Waziri wa usalama wa Israel Gilad Erdan amesema wanatekeleza uamuzi wa mahakama kuu iliyoamua kwamba majengo hayo yamejengwa kinyume cha sheria karibu na uzio huo kwa hivyo ni hatari kwa raia na jeshi. Palestina wamekanasha hilo wakisema uzio huo umegawanya sehemu hizo na kwa hivyo wao wamejenga sawa katika eneo lao la Jerusalem.
Wanajeshi 200 wamehusika
Kulingana na waziri Gilad, Polisi mia saba na wanajeshi 200 wamehusika katika kuvunja nyumba hizo. Mmoja wa waliobomolewa nyumba zao ni Fadi Al-Wahash - jumba lake la ghorofa tatu lililokuwa linaendelea kujengwa limevunjwa, Fadi anasema kwamba amekuwa akiijenga pole pole ghorofa hiyo baada ya kupata kibali kutoka kwa mamlaka ya Palestine ila leo amepoteza kila kitu.
Juma lililopita Umoja wa Mataifa uliitaka Israel kutoendelea na mpango wake wa kuvunja majengo ya Wapalestina. Umoja wa Mataifa ulieleza kwamba kutekeleza mpango huo kutasabaisha hasara kwa watu 350 ambao majengo yao yanaendelea kujengwa vile vile kusababisha watu kukosa makao. Ubomoaji huo ni mzozo mpya katika eneo hilo la Jerusalem linalokaliwa na zaidi ya Waisraeli laki tano na Wapalestina laki tatu. Vile vile ndiko kulikuwa na majengo matakatifu ya Waisilamu, Wakristo na Wayahudi.
(DPAE/RTRE)