ISTANBUL:Erdogan ahidi mabadiliko kuifanya Uturuki iingie EU
24 Julai 2007Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameahidi kuendeleza mfumo wa uongozi usiegemea upande wa dini na kufanya mageuzi makubwa, baada ya chama chake cha kiislam kushinda uchaguzi wa Bunge wa Jumapili.
Matokeo ya awali yanakipa ushindi wa asilimia 47 chama hicho cha AKP, lakini chama hicho kimeshinda viti 340 kati ya viti 550 vya bunge, ikiwa ni karibu mara mbili zaidi ya chama hasimu.
Umoja wa Ulaya umemtaka Erdogad kuendelea na mageuzi yanayotakiwa ili kufikia kiwango cha kuwa mwanachama wa Umoja huo wa Ulaya.
Waziri Mkuu huyo wa Uturuki pia alitoa wito wa kuchaguliwa kwa mgombea wa chama hicho ambaye alikatiliwa na vyama visivyoegemea upande wa dini kuwa rais wa nchi hiyo.
Chama cha AKP kwa sasa kinawajibika kutafuta muafaka juu ya mgombea wa nafasi hiyo ya urais na pia kuangalia uwezekano wa kutuma majeshi yake kaskazini mwa Irak kuwasambaratisha waasi wa Kikurd wenye asili ya Kituruki waliyoko katika eneo hilo.